Fenerbahce, Uturuki
Kocha mkuu wa klabu ya Fenerbahce ya Uturuki, José Mourinho amesema kwamba hafuti uwezekano wa kuinoa klabu ya Real Madrid kwa mara ya pili.
Mourinho, 61, aliwahi kuinoa Real Madrid kwa misimu mitatu kuanzia mwaka 2010 na kuiwezesha timu hiyo kubeba mataji ya La Liga, Copa del Rey na Spanish Supercup.
Kocha huyo alikuwa akijibu swali aliloulizwa kama kuna siku itatokea atakuwa tayari kuwa kocha wa Real Madrid kwa mara nyingine naye akasema hilo linawezekana.
“Wakati wote nitakuwa shabiki mkubwa wa Real Madrid, wana kocha bora duniani, rafiki yangu Carlo (Ancelotti) na anafanya kazi yake vizuri.
Mourinho pia alisema Rais wa Real Madrid, Florentino Perez ndiye atakayeamua mambo ya baadaye ya klabu hiyo kuhusu aina ya kocha wanayemhitaji.
“Kama wanataka kocha kijana mwenye mipango mikubwa kama Xabi Alonso au kuendelea na kocha wa aina ya Ancelotti ambaye ni mzoefu au kuangalia katika makocha wa kikosi cha akiba hapo yupo Raul au kutoka timu ya vijana kwa Alvaro Arbeloa,” alisema Mourinho.
Alonso, kiungo wa zamani wa Real Madrid kwa sasa ni kocha wa Bayer Leverkusen amekuwa akitajwa zaidi na kupewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi ya Ancelotti iwapo Madrid itaachana na kocha huyo.
Ancelotti, 65 ana mkataba na Real Madrid ambao utafikia ukomo Juni 2026 huku Mourinho akiamini kuwa Perez atafanya maamuzi sahihi iwapo atahitajika kocha wa kuchukua nafasi ya Ancelotti.
Mourinho kabla ya Fenerbahce na Real Madrid, pia amewahi kuzinoa timu za FC Porto, Chelsea, Inter Milan, Tottenham, Man United na AS Roma.
Kimataifa Mourinho ajipigia debe Real Madrid
Mourinho ajipigia debe Real Madrid
Read also
