Na mwandishi wetu
Yanga imekamilisha usajili wa beki Israel Mwenda kutoka Singida Black Stars ikiwa siku nne zimebaki kabla ya kufunguliwa rasmi dirisha dogo la usajili Desemba 15 mwaka huu.
Mwenda aliyekuwa akiichezea Simba kabla ya kutua Singida BS ambayo amejiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu amejiunga na timu hiyo kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu.
Beki huyo wa kulia ambaye pia amewahi kutamba na timu za KMC na Alliance FC inaaminika kuwa anajiunga na Yanga au Wananchi kwa lengo la kuimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Mwenda ambaye inadaiwa uamuzi wake wa kukubali kuondoka Simba ulitokana na kutopata muda wa kutosha katika kikosi cha kwanza kwa kuwa nafasi aliyokuwa akiichezea pia anacheza Shomary Kapombe.
Ubora wa Kapombe kuanzia msimu uliopita ndiyo sababu kubwa iliyomuweka katika wakati mgumu Mwenda hadi kuhamia Singida BS lakini sasa katika Yanga atakuwa na kazi ya kuwania namba mbele ya Yao Kouassi.
Yanga pia inadaiwa kumchukua beki huyo ili awasaidie kukabiliana na janga la majeruhi hasa katika beki ya kulia pamoja na ile ya kushoto ambayo amekuwa akicheza Shedrack Boka.
Kwa kuwa Mwenda pia ana uwezo wa kucheza upande wa kushoto inaelezwa kuwa atakuwa msaada akikosekana Boka ambaye naye katika siku za karibuni ameandamwa na janga la kuwa majeruhi.
Yanga katika siku za karibuni imekuwa na tatizo la nafasi za beki wa kulia na kushoto ambapo licha ya ubora wa Yao na Boka lakini inapotokea kuumia kwa mmoja kati yao pengo linaonekana wazi.
Usajili wa Mwenda kwa mantiki hiyo unatajwa kuangalia zaidi maeneo hayo hasa kwa mapungufu ambayo yamekuwa yakionekana katika mechi ambazo mmoja kati ya Yao na Boka anapokuwa majeruhi.
Kwa hali hiyo Mwenda anaweza kujikuta katika tatizo lile lile lililomtoa Simba la kukosa nafasi ya uhakika kwani upande wa kulia anaoumudu zaidi unamilikiwa na Yao ambaye ubora wake unajulikana.
Yao akiwa katika ubora wake ni vigumu kumuweka benchi kama ambavyo Kibwana Shomari ambaye anamudu beki ya kulia lakini ameshindwa kuwa na namba mbele ya Yao.
Soka Israel Mwenda sasa Mwananchi
Israel Mwenda sasa Mwananchi
Read also
