Na mwandsishi wetu
Baada ya kuanza vizuri mechi ya Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika, Simba Jumapili hii imekuwa mbaya kwa timu hiyo baada ya kuchapwa mabao 2-1 mbele ya SC Constantine ya Algeria.
Kabla ya mechi dhidi ya Constantine, Simba ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bravos du Maquis ya Angola na kuibua matumaini ya kuendelea kufanya vyema kwenye michuano hiyo.
Simba walioukuwa ugenini kwenye Uwanja wa Mohamed Hamloui, waliuanza mchezo wao na Constantine kwa kasi na katika dakika ya 24 walipata bao la kwanza lililofungwa na nahodha Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’.
Zimbwe akiwa pembeni alipiga krosi baada ya kushirikiana vyema na Jean Ahoua na mpira kumshinda kipa wa Constantine, Kheireddine Bousouf ambaye katika jitihada za kuokoa alijikuta akiuzamisha wavuni.
Simba waliendelea kucheza soka la kujiamini wakifanya mashambulizi na kujihami na hadi dakika 45 za kwanza zinakamilika, Simba walikuwa mbele kwa bao hilo moja.
Kipindi cha pili, wenyeji Constantine walibadilika kwa kiasi kikubwa na kulisakama lango la Simba mara kwa mara na haikushangaza walipopata bao la kusawazisha dakika ya tatu baada ya mapumziko.
Bao hilo la Constantine walizawadiwa na beki wa Simba, Abdulrazack Hamza ambaye alijikuta akifunga katika jitihaza za kuokoa shambulizi.
Kabla Simba hawajajipanga vizuri walijikuta wakipachikwa bao la pili katika dakika ya 50, bao lililofungwa na Brahim Dib.
Kipigo cha Simba kinaifanya Algeria iwe nchi ngumu kwa timu za Tanzania kwa siku za karibuni baada ya Jumamosi Yanga nao kulala kwa mabao 2-0 mbele ya MC Alger katika mechi ya Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika
Baada ya Simba kuchezea kichapo, Constantine sasa wanashika usukani wa kundi lao wakiwa na pointi sita nyuma yao wapo Bravos du Maquis ambao waliwafunga CS Sfaxien mabao 3-2 na Simba wanashika nafasi ya tatu na pointi zao tatu.
Simba sasa wanajiandaa kucheza dhidi ya CS Sfaxien wanaoshika mkia katika kundi hilo, mechi itakayopigwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kimataifa Simba yajeruhiwa Algeria
Simba yajeruhiwa Algeria
Read also
