Liverpool, England
Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah amesema ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-0 wa jana Jumamosi dhidi ya Man City ni mechi ya mwisho kwake kuivaa timu hiyo kwenye dimba la Anfield.
Kauli ya mchezaji hiyo inaashiria kwamba ataihama timu hiyo huku habari zaidi zikidai kwamba vigogo wa klabu ya PSG ya Ufaransa wako katika mkakati mzito wa kumsajili mchezaji huyo.
Katika mechi ya jana Salah ndiye aliyetoa pasi iliyozaa bao la kwanza la Liverpool lililofungwa na Cody Gakpo na baada ya hapo akafunga bao la pili kwa penalti iliyotolewa baada ya Luis Diaz kuchezewa rafu na Stefan Ortega.
Ushindi huo umeifanya Liverpool kushika usukani katika Ligi Kuu England (EPL) ikiwa mbele kwa tofauti ya tisa na kuwaacha Man City ambao ni mabingwa watetezi kwa tofauti ya pointi 11.
Mara baada ya mechi hiyo Salah aliulizwa kuhusu mambo ya baadaye ndani ya Liverpool na kukiri kwamba huenda hiyo ikawa mechi yake ya mwisho dhidi Man City huku mkataba wake na Liverpool ukifikia ukomo mwishoni mwa msimu huu.
“Ukweli ni kwamba haya ni mambo yangu, hadi sasa hii ndiyo mechi yangu ya mwisho kuichezea Liverpool dhidi ya Man City kwa hiyo nilienda kuifurahia, mazingira yalikuwa ya kuvutia, hivyo naifurahia kila hatua, ni matumaini kwamba tutashinda taji la ligi na baada ya hapo mengine yatafuata,” alisema Salah.
Akifafanua zaidi kuhusu hatma yake ndani ya kikosi cha Liverpool Salah alisema kwamba huu ni mwezi Desemba na hajapata ofa yoyote ya kubaki katika klabu hiyo kwa hiyo huenda yeye ni wa kuondoka zaidi kuliko wa kubaki.
“Mnajua nimekuwa katika klabu hii kwa miaka mingi, hakuna klabu kama hii lakini mwisho wa siku si suala langu peke yangu, na kama nilivyosema hii ni Desemba na hakuna lolote lililofanyika kuhusu mambo yangu ya baadaye katika klabu hii,” alisema Salah.
Salah pia amekuwa akihusishwa kwenda kucheza soka Saudi Arabia ingawa PSG ndio wanaotajwa zaidi kuisaka saini ya mshambuliaji huyo kwa imani kwamba watamsajili baada ya msimu huu akiwa mchezaji huru.
