Manchester, England
Nafasi ya kocha Erik ten Hag katika kikosi cha Man United imeendelea kujadiliwa huku makocha Xavi Hernandez na Ruben Amorim (pichani chini) wa Sporting Lisbon wakianza kutajwa.
Hii si mara ya kwanza kwa Xavi aliyeachana na Barcelona msimu uliopita kutajwa akihusishwa na nafasi hiyo lakini kwa Amorin hii ni mara yake ya kwanza kuingizwa katika mbio hizo.
Habari za ndani zilizopatikana kwenye vyanzo mbalimbali vya habari hii leo Jumamosi vimeeleza kuwapo kwa mpango huo ingawa makocha hao hawajasema lolote kuhusu kuhusishwa kwao.
Kilichopo wazi kwa Ten Hag ni kwamba mwenendo wa Man United si wa kuvutia katika Ligi Kuu England (EPL) hivyo mjadala kuhusu hatma ya kocha huyo ni jambo linalotarajiwa.

Mara baada ya msimu uliopita wa 2023-24 kumalizika ilitarajiwa ingekuwa mwisho wa Ten Hag kuinoa Man United lakini ubingwa wa Kombe la FA inasemekana ulimbeba na kuwafanya vigogo wa timu hiyo kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja.
Katika EPL hadi sasa Man United inashika nafasi ya 12 ikiwa imecheza mechi nane, imepoteza tatu na kushinda mitatu na kutoka sare mara mbili.
Na ingawa kocha huyo amekuwa akijifariji mara kwa mara kutokana na janga la wachezaji majeruhi kwenye kikosi chake lakini kiujumla hali halisi hairidhishi na haishangazi kuona nafasi yake ikizidi kugeuzwa mjadala.
