Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imejiweka pagumu katika harakati za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 baada ya kulala kwa mabao 2-0 mbele ya DR Congo.
Katika mechi hiyo iliyopigwa leo Jumanne Oktoba 15, 2024 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, matokeo hayo yanaifanya DR Congo ifuzu moja kwa moja Afcon ikifikisha pointi 12 baada ya kushinda mechi zake zote nne hadi sasa.
Stars katika mechi ya leo licha ya kukabiliana vyema na DR Congo lakini ilizama kwa mabao ya dakika za 87 na 90 yaliyofungwa na Elia Meshack, mabao yaliyofifisha matumaini ya Stars.
Kwa matokeo hayo Stars inakuwa imelala mara mbili mbele ya DR Congo baada ya kufungwa bao 1-0 ugenini katika mechi iliyopigwa Oktoba 10 na sasa ili kufufua matumaini ya kufuzu Afcon inatakiwa kufanya vizuri mechi zake mbili zilizobaki.
Stars iliyo katika Kundi H inasubiri kuumana na Guinea kwenye uwanja wa nyumbani hiyo ni baada ya kushinda ugenini katika mechi yake ya awali dhidi ya timu hiyo kwa mabao 2-1.
Timu hiyo pia inatakiwa kushinda mechi yake nyingine dhidi ya Ethiopia baada ya sare ya bila kufungana katika mechi ya awali baina ya timu hizo.
Kimataifa Stars yajiweka pagumu Afcon 2025
Stars yajiweka pagumu Afcon 2025
Read also
