Atlanta, Marekani
Nyota wa zamani wa mpira wa kikapu nchini Marekani, Dikembe Mutombo (pichani) amefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani (kansa) ya ubongo akiwa na miaka 58.
Kwa mujibu wa NBA, Mutombo amefariki jana Jumatatu Septemba 30 ikiwa takriban miaka miwili imepita tangu ndugu zake watoe taarifa kuwa nyota huyo alikuwa katika matibabu ya saratani.
“Kwenye dimba la mpira wa kikapu alikuwa ni mmoja wa wazuiaji mahiri na mlinzi bora katika historia ya NBA, nje ya mpira wa kikapu alikuwa mtu mwenye moyo wa kuwasaidia wengine,” alisema Kamishna wa NBA, Adam Silver.
Silver alisema kwamba hakuna mtu ambaye alikuwa na sifa za kuwa balozi wa dunia wa NBA zaidi ya Mutombo kwani alikuwa ni mtu mwenye ubinadamu wa hali ya juu.
Ni mtu aliyependa kuona kile ambacho mpira wa kikapu ungekifanya kwa kuleta matokeo chanya katika jamii hasa kwa jamii yake ya asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na bara la Afrika kwa ujumla.
“Nimekuwa mwenye bahati ya kusafiri sehemu mbalimbali duniani na Mutombo na nikaona jinsi alivyokuwa muungwana na mwenye shauku ya kuwainua watu, wakati wote alikuwa mwenye kupatikana katika matukio ya NBA,” alisema Silver.
Katika mpira wa kikapu, Mutombo alizoeleka kwa namna alivyoutumia vyema urefu wake wa futi saba na alipenda kuinua kidole chake cha mkono wa kulia juu baada ya kuzuia mipira iliyoelekezwa katika timu yake.
Wakati wa uhai wake alicheza misimu 18 ya NBA akiwa na timu za Houston Rockets, Philadelphia 76ers, Atlanta Hawks, Denver Nuggets, New Jersey Nets, New York Knicks kabla ya kustaafu baada ya msimu wa 2008-09.
Mutombo ambaye pia ni kati ya wachezaji mpira wa kikapu bora walioingia katika Basketball Hall of Fame, anazungumza lugha tisa, mwaka 1997 alianzisha taasisi ya Dikembe Mutombo Foundation ambayo inatoa misaada ya kuboresha huduma za afya na hali za maisha kwa watu wa DR Congo.
Kupitia taasisi hiyo, Mutombo amewezesha kujengwa hospitali yenye vitanda 170 mjini Kinshasa, hospitali ambayo imetoa huduma kwa watu zaidi ya nusu milioni wakiwamo wenye uwezo mdogo kiuchumi.
