New York, Marekani
Aliyewahi kuwa kocha wa Tottenham Hotspur na Chelsea, Mauricio Pochettino ametangazswa kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya taifa ya soka ya wanaume ya nchini Marekani.
Pochettino anachukua nafasi iliyoachwa na Gregg Berhalter ambaye Julai mwaka huu alifutwa kazi baada ya Marekani ikiwa mwenyeji wa fainali za Copa America kutolewa katika hatua ya makundi.
Uamuzi wa kumpa kazi Pochettino ambaye anatokea Argentina ulifikiwa kabla ya timu hiyo kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na New Zealand ambapo kocha huyo alisema amepata fursa ambayo asingeweza kuikataa.
“Uamuzi wa kujiunga na timu Marekani kwangu si tu unahusu soka bali ni kushiriki safari ambayo nchi hii pamoja na timu zinaifanya. Nguvu, matamanio na hasira za kufanikisha mambo ni vitu vyenye historia hapa, hayo ndiyo yaliyonishawishi,” alisema Pochettino.
Alisema Marekani nchi ambayo itakuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2026, analiona kundi la wachezaji wenye vipaji na fursa tele na pamoja watatengeneza kitu cha kipekee ambacho kitaifanya nchi nzima iwe na la kujivunia.
Naye Mkurugenzi wa Soka Marekani, Matt Crocker ambaye ndiye aliyeongoza mchakato wa kumsaka kocha wa kuchukua nafasi ya Berhalter, alitumia muda mwingi akiwa Southampton wakati Pochettino akkiwa kocha.
Crocker alimtaka Pochettino kuwa ni kocha mshindi aliye na matamanio katika maendeleo ya wachezaji na amethibitisha uwezo wake wa kujenga timu imara na za ushindani.
Pochettino alijiunga na Southampton akitokea Espanyol kabla ya kujiunga na Spurs ambayo mwaka 2019 aliifikisha hatua ya fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya na baada ya hapo alizinoa PSG na Chelsea.
