Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema mshambuliaji wake, Erling Haaland hazuiliki msimu huu wa 2024-25 baada ya kupiga hat trick mbili katika mechi tatu.
Kwa Haaland hiyo inakuwa rekodi yake mpya katika Ligi Kuu England (EPL), rekodi ambayo inatoa kila dalili za mambo mazuri zaidi mbele ya safari.
Kabla ya kuanza msimu huu wa EPL, Pep alisema kwamba hana uhakika na kikosi chake lakini jambo analoweza kuwa na uhakika nalo kwa sasa ni timu yake kuwa na mpachika mabao anayeweza kubadili matokeo.
Baada ya kufunga hat trick katika mechi iliyopita na Ipswich Town ambayo Man City ilitoka na ushindi wa 4-1, juzi Jumamosi timu hiyo ilipata ushindi wa 3-1 dhidi ya West Ham huku Haaland akifunga mabao hayo matatu ya timu yake.
Akimzungumzia Haaland, Pep alisema anadhani mabeki hawakuwa tena na uwezo wa kumzuia Haaland kutupia nyavuni akitolea mfano moja ya mabao katika mechi na West Ham kwamba hata beki angekuwa na ‘bunduki’ asingeweza kumzuia.
“Hakuna beki wa kati ambaye angeweza kumzuia hata kama angekuwa na bunduki, ni vigumu, ilikuwa kasi kubwa na kwa nguvu sana,” alisema Pep.
Haaland, 24, hadi sasa ana rekodi ya hat trick 11 akiwa na Man City na anakuwa mchezaji wa pili katika historia ya EPL kufunga hat trick mara mbili mfululizo baada ya Harry Kane.
Msimu uliopita ulikuwa mgumu kidogo kwa Haaland baada ya kuwa majeruhi japo alimaliza akiwa mfungaji bora na mabao yake 27 lakini anasema kwamba amepata muda mrefu wa kupumzika na hilo ni jambo zuri kwake.
“Najisikia vizuri, nimepata nguvu, nimekuwa na mapumziko marefu, miaka ambayo nimekuwa hapa ilikuwa inakwenda kasi mno, lakini kwa sasa nimepata wasaa wa kuupumzisha mwili pamoja na miguu, na sasa niko tayari kwa mambo mengi zaidi,” alisema Haaland.
Kimataifa Pep: Hakuna wa kumzuia Haaland
Pep: Hakuna wa kumzuia Haaland
Read also
