Monaco, Ufaransa
Nahodha na winga wa timu ya Al Nassr ya Saudi Arabia, Cristiano Ronaldo amesema kwamba milango bado ipo wazi kwa upande wake kucheza Ligi ya Mabngwa Ulaya kwa mara nyingine.
Kauli ya Ronaldo nyota wa zamani wa timu za Man United, Real Madrid na Juventus imekuja baada ya mchezaji huyo kuhusika katika droo ya mfumo mpya wa michuano hiyo kwa msimu huu wa 2024-25 iliyofanyika jana Alhamisi.
Ronaldo ambaye pia amewahi kuichezea klabu ya Sporting Lisbon ya Ureno katika tukio hilo pia alipewa tuzo ya kuwa mfungaji mwenye rekodi ya mabao mengi (140) katika historia ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Alipotaniwa na rais wa Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa), Aleksander Ceferin kwa kutocheza tena Ligi ya Mabingwa, Ronaldo hakufuta moja kwa moja uwezekano wa siku moja kurudi kwenye michuano hiyo.
“Usisahau kwamba nacheza Asia (Ligi ya Mabingwa), kwangu ni furaha kubwa kuwa hapa, asante kwa tuzo hii ya kipekee, ina maana kubwa kwangu,” alisema Ronaldo.
“Kama unavyofahamu, Ligi ya Mabingwa ni michuano ya juu kwenye soka, nimewahi si tu kupata fursa katika michuano hiyo, si wewe tu unayefahamu bali rekodi zinazungumza lakini simaanishi hilo bali namaanisha furaha ya kucheza katika michuano hii, ni hamasa kubwa,” alisema Ronaldo.
Akifafanua uwezekano wa kurudi katika michuano hiyo, Ronaldo ambaye amebeba taji la michuano hiyo mara tano, mara nne na Real Madrid na mara moja na Man United alisema, “katika soka huwezi kujua nini kitatokea, ngoja tuone yajayo yatakavyokuwa.”
