Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema ratiba ngumu ya msimu huu inawafanya wafikirie kuwapa muda wa mapumziko mchezaji mmoja mmoja ili kuwaepusha na uchovu uliopitiliza.
Real Madrid ilizianza mbio za msimu wa 2024-25 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Atalanta katika Uefa Super Cup kabla ya kuivaa Mallorca katika mechi ya kwanza ya La Liga.
Wachezaji wa Real Madrid katika msimu huu wanatarajia kupambana kuwania mataji saba kuanzia La Liga, Kombe la Mfalme, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Uefa Super Cup, Spanish Super Cup, Kombe la Dunia la Klabu na mashindano mapya ya kuwania taji la mabara.
Michuano ya Kombe la Dunia la Klabu yailiyofanyiwa mabadiliko yanatarajia kuanza majira ya kiangazi nchini Marekani ingawa siku maalum ya kuanza michuano hiyo pamoja na viwanja yote hayo bado hayajawekwa wazi na hiyo maana yake ni kwamba msimu huu kwa Real Madrid utafikia ukomo Juni 2025.
“Kuna mambo tunayafanyia tathmini, wachezaji wanahitaji kupumzika, wanahitaji kulfurahia maisha (kula bata), tunafikiria wakati msimu ukiendelea tunaweza kumpa mchezaji mmoja mmoja wiki ya kupumzika,” alisema Ancelotti.
Akifafanua zaidi Ancelotti alisema mchezaji anaweza asionekane kwenye mechi kwa wiki moja na akapewa muda huo ili apumzike na familia yake na kwamba jambo hilo litafanywa zaidi kwa wachezaji walio kwenye timu za taifa na ushauri wa jopo la madaktari wa timu utazingatiwa.
Ancelotti katika hilo alimtolea mfano mshambuliaji wa timu hiyo ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Brazil, Vinicius Junior ambaye alisema kwa kalenda ya mchezaji huyo ni muhimu akawa na muda wa mapumziko katikati ya msimu.
