Chicago, Marekani
Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca ametetea uamuzi wa kumpa unahodha Enzo Fernandez katika mechi ya kirafiki na Real Madrid akisema suala hilo liko wazi kwa kuwa mchezaji huyo anaheshimika katika kikosi cha timu hiyo.
Fernandez (pichani juu), ambaye pia ni kiungo wa timu ya taifa ya Argentina, alipewa kitambaa cha unahodha wakati wa kipindi cha pili, mechi ambayo Chelsea ililala kwa mabao 2-1.
Uamuzi wa kumpa mchezaji huyo kitambaa cha unahodha umeacha maswali kwani anakumbukwa kwa kuandamwa na kashfa ya ubaguzi wa rangi iliyoibuka katika timu yake ya taifa.
Wakati akishangilia ushindi wa Argentina kwenye Copa America, Enzo, 23, alitupia picha ya video iliyomuonesha akiwa na wachezaji wenzake wa timu ya taifa wakiimba nyimbo ya kuwadhihaki wachezaji wa Ufaransa wenye asili ya Afrika.
Zaidi ya hilo, Fernandez pia amepewa jukumu hilo kutoka kwa Reece James ambaye hapo kabla alinukuliwa akisema kwamba alichokifanya Fernandez kinaweza kusababisha matatizo miongoni mwa wachezaji wa Chelsea.
Beki wa Chelsea, Wesley Fofana alichukizwa na video hiyo wakati klabu ya Chelsea ilitoa taarifa ya kulaani kitendo kilichofanywa na Fernandez.
Baada ya kitendo hicho Fernandez aliomba radhi ingawa Maresca alimtetea akisema kwamba mchezaji huyo hakuwa na nia mbaya katika tukio hilo.
“Niwe tu mkweli nafikri tulipombadili Reece tuliamua kumpa kitambaa cha unahodha Enzo, na hii inaonesha jinsi anavyoheshimika katika kikosi, nafikiri hilo lipo wazi,” alisema Maresca.
Chelsea Jumapili inatarajia kucheza na Inte Milan katika mechi ya kirafiki ambayo inatarajia kuwa ya mwisho kabla ya kuanza rasmi msimu wa 2024-25 ambapo itauanza kwa mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Man City.
