Na mwandishi wetu
Kocha wa Simba, Fadlu Davids hana presha yoyote katika mechi dhidi ya Yanga maarufu Dar Derby itakayochezwa kesho Alhamisi kwani wataichukulia kama mechi nyingine yoyote lengo likiwa kupata ushindi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumatano kocha huyo kutoka Afrika Kusini licha ya kutoa kauli hiyo lakini alikiri kwamba mechi hiyo itawapa kipimo cha ukweli kuhusu soka la Tanzania.
“Tunacheza na Yanga ambao ni mabingwa na hiyo itatupa kipimo cha kweli kuhusu soka la Tanzania ingawa mechi hii haiwezi kutoa mtazamo wa timu yetu itakavyokuwa kwenye ligi,” alisema David.
Alisema kwamba mechi ya Simba Day dhidi ya APR ambayo walishinda kwa mabao 2-0 iliwapa mtazamo wa namna timu yao ilivyokuwa baada ya maandalizi ya wiki nne za kujiandaa na msimu mpya wa 2024-25.
David pia alisema kwamba Yanga tayari imekuwa vizuri kwa miaka mitatu na ina kocha ambaye tayari ana mwaka mmoja kwenye timu lakini Simba bado mpya ikiwa na wiki nne za kuwa pamoja.
Alifafanua kwamba halikuwa jambo rahisi kuwaingiza katika mfumo wachezaji wapya 14 kwenye timu mpya ambayo imekuwa pamoja kwa kipindi cha wiki nne.
Naye kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kwamba timu yake haipaswi kufanya makosa katika mechi hiyo badala yake wanapaswa kuwa makini kila idara kwa sababu ni mechi ya mtoano.

Alisema anawaheshimu Simba hasa kwa kuwa mechi za derby hakuna timu inayotajwa kuwa dhaifu kwa kuwa ni mechi maalum na anafahamu kwamba wapinzani wao Simba wana timu mpya na hivyo wataitumia mechi hiyo kuonesha ubora wao.
Yanga na Simba zitaumana katika mechi hiyo ambayo ni ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa ambapo katika mechi nyingine Azam FC itatoana jasho na Coastal Union kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.




Washindi wa mechi hizo watachuana katika mechi ya fainali kumpata mshindi wa Ngao ya Jamii, michuano ambayo inaashiria kufunguliwa kwa pazia la msimu mpya wa soka wa 2024-25 nchini Tanzania.
