Charlotte, Marekani
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema nafasi na majukumu ya Jude Bellingham katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid hayatobadilika licha ya klabu hiyo kumsajili, Kylian Mbappe.
Bellingham, 21, ambaye pia ni kiungo wa timu ya taifa ya England katika msimu wake wa kwanza na Real Madrid wa 2023-24 amebeba vyema majukumu yake akifunga mabao 23 katika mechi 42 na timu hiyo kubeba mataji ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika msimu mpya wa 2024-25, Real Madrid imemsajili Mbappe, 25, ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Ufaransa, usajili ambao inadhaniwa unaweza kumfanya Ancelotti ambadilishie Bellingham majukumu yake kwenye kikosi cha kwanza.
Ancelotti hata hivyo alikana kuwa na mpango wowote wa kumbadilishia majukumu Bellingham kwa kumsogeza mbele zaidi ili Mbappe aingie vyema katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Kocha huyo badala yake alisisitiza kwamba hakuna kitakachobadilika kwa mchezaji huyo ambaye pia aliwahi kunukuliwa akisema kwamba kucheza timu moja na Mbappe litakuwa jambo zuri.
“Msimu wa kwanza tu ameshangaza kweli kwa sababu ameonesha kiwango cha kipekee, amekuwa bora, msimu ujao hautokuwa tofauti, atakuwa mmoja wa wachezaji bora tulio nao, anaisaidia sana timu kwa kiwango chake,” alisema Ancelotti.
Ancelotti pia alimtetea Bellingham baada ya mchezaji huyo kushutumiwa kwa kiwango kisichovutia kwenye fainali za soka za Euro 2024 zilizomalizika hivi karibuni nchini Ujerumani ambapo England ilifikia hatua ya fainali lakini ilishindwa kutamba mbele ya Hispania waliobeba kombe.
“Hayo ni mawazo tu lakini Bellingham alicheza vizuri kwenye Euro, England pia ilicheza vizuri hasa hadi kufikia hatua ya fainali na ilikuwa bado kidogo wabebe kombe,” alisema Ancelotti.
Mbappe na Bellingham ambao wote walikuwa na timu zao za taifa kwenye fainali za Euro 2024 wanasubiriwa kwa hamu kuibeba Real Madrid katika msimu mpya wa 2024-25 unaotarajia kuanza kutimua vumbi baadaye mwezi huu.
