New York, Marekani
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema Jadon Sancho anaweza kuuanza msimu mpya wa 2024-25 akicheza nafasi ya mshambuliaji wa kati namba 9 kuziba nafasi ya Rasmus Hojlund ambaye ni majeruhi.
Hojlund anatarajia kuwa nje ya uwanja kwa wiki takriban sita baada ya kuumia misuli katika mechi ya kwanza ya kirafiki nchini Marekani dhidi ya Arsenal.
Baada ya kuumia kwa Hojlund, Ten Hag katika mechi dhidi ya Real Betis akampa nafasi Sancho ambaye amekuwa nje ya kikosi hicho kwa miezi 10 tangu kukorofishana na kocha huyo.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumatano na Man United kutoka na ushindi wa mabao 3-2, Sancho alicheza namba 9 na baada ya hapo akacheza mechi nyingine jana Jumamosi dhidi ya Liverpool ambayo Man United ililala kwa mabao 3-0.
Ten Hag amesema kwamba Sancho sasa anaweza kuanza kama mshambuliaji wa kati katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Man City itakayopigwa wiki ijayo.
Kocha huyo aliongeza kuwa Sancho ambaye baada ya kuondoka Man United aliuzwa kwa mkopo katika klabu ya Borussia Dortmund, pia anaweza akacheza nafasi hiyo hiyo katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Fulham badala ya Joshua Zirkee ambaye ni usajili mpya.
“Ni kweli kwamba tunaye Jadon kama mshambuliaji, tunajua anaweza kucheza pembeni lakini pia anamudu nafasi ya ‘mshambuliaji feki’ nafasi zote hizo anaweza kutumika,” alisema Ten Hag
Mchezaji mwingine ambaye anaweza kumudu nafasi ya Hojlund ni Marcus Rashford lakini Ten Hag amebainisha kuwa Rashford ataendelea na majukumu yake ya nafasi ya ushambuliaji akitokea upande wa kushoto.
