Los Angeles, Marekani
Beki wa Man United Jonny Evans (pichani) amesema limekuwa jambo gumu mno kwake kuona wafanyakazi 250 wa klabu hiyo wanaachishwa kazi katika mpango wa kubana matumizi.
Sehemu kubwa ya wafanyakazi wa Man United wamearifiwa kupunguzwa kazi ikiwa ni mpango maalum wa kampuni ya INEOS chini ya Sir Jim Ratcliffe, ambao ni wamiliki wenza wapya wa klabu hiyo.
Evans, 36, ambaye amekuwa karibu na klabu hiyo tangu akiwa na miaka tisa amesema kwamba kwake anaona kipindi hiki kuwa kigumu kutokana na uamuzi huo unaogusa sehemu kubwa ya wafanyakazi.
“Watu wengi wamepoteza kazi katika wiki chache zilizopita, imekuwa tabu na jambo gumu kwangu kuona likifanyika, wamiliki wapya wanaona ndio mwelekeo sahihi wanaotaka kwenda, lakini unajua pia si jambo rahisi kwa kila mmoja wetu,” alisema Evans.
“Kuna watu nimekuwa nikiwafahamu kwa miaka 20 na jambo hili limetokea wakati tukiwa kwenye ziara ya mbali, kwa hiyo wengi wetu tumekuwa gizani, najua kila kitu kitafanyiwa kazi, mambo yatakuwa sawa tutakaporudi,” alisema Evans.
Kwa Evans ana historia ndefu Man United tangu ajiunge rasmi kwenye timu ya wakubwa mwaka 2007 wakati huo akiwa na miaka 19 akitokea kwenye akademi ya klabu hiyo.
Kaka yake Evans aitwaye Corry pia alikuwa akiichezea Man United wakati mkewe, Helen pia anafanya kazi Man United kwenye televisheni ya klabu hiyo wakati baba yake Jackie naye alifanya kazi kwenye akademi ya klabu hiyo akiwa kocha.
“Watu ambao umewafahamu kwa muda mrefu, muda mrefu mno, jambo moja kuhusu kufanya kazi katika klabu kama Man United, wote mnakuwa wamoja na kila mtu wakati wote mnakuwa mpo naye, wanaoachishwa kazi ni wengi, lakini nafikiri huu ni utamaduni wa klabu,” alisema Evans.
Katika mpango huo wa kupunguza wafanyakazi 250, wachezaji na maofisa wa kikosi cha kwanza hawajaguswa ingawa Evans anasema kwamba bado tukio hilo limeendelea kuwa mjadala kwenye timu wakati huu wakiwa ziarani Marekani.
