Saint-Etienne, Ufaransa
Kocha wa Argentina, Javier Mascherano (pichani) amelielezea kuwa ni fedheha tukio la timu yake kufungwa mabao 2-1 na Morocco kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris baada ya kuibuka vurugu uwanjani.
Mashabiki waliingia katika vurugu na kusababisha mechi ya kwanza ya soka ya Michezo ya Olimpiki inayoendelea nchini Ufaransa kusimamishwa kwa takriban saa mbili kabla ya kuendelea na mechi kumalizika bila mashabiki uwanjani.
Wakati Morocco ikiwa mbele kwa mabao 2-1, Argentina ilionekana kupambana kusaka bao la kusawazisha dakika 16 baada ya kuanza kipindi cha pili kabla ya chupa kuanza kurushwa uwanjani na mashabiki wenye jezi za Morocco kuvamia uwanja.
Kutokana na hali hiyo mwamuzi alizitaka timu kutoka uwanjani wakati huo saa 10 jioni kabla ya kuzirudisha saa mbili baadaye wakati huo mashabiki wameshatolewa kwenye Uwanja wa Geoffroy-Guichard ilipochezwa mechi hiyo.
Muda mfupi kabla ya mechi hiyo kusimama, Argentina walipata bao ambalo hata hivyo lilikataliwa kwa madai kwamba mfungaji aliotea baada ya waamuzi kujiridhisha kupitia VAR.
“Sijawa kocha wa kipindi kirefu lakini katika maisha yangu ya soka nikiwa mchezaji sijawahi kuona tukio kama hili,” alisema Mascherano ambaye akiwa mchezaji wa timu ya taifa ya Argentina walibeba medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2004 na 2008.
“Ni jambo lisiloeleweka, lakini ndivyo ilivyokuwa hatukuweza kuwadhibiti, nimeshawaambia vijana kwamba sasa tunatakiwa kuangalia mbele, kuzisaka pointi sita ambazo zitatuwezesha kufuzu na hilo litatupa nguvu na hasira ya kukabiliana na kile kilicho mbele yetu,” alisema Mascherano.

Mascherano, kiungo wa zamani wa Argentina alisema awali manahodha wa timu zote waliamua mechi isiendelee na baadaye waandaaji wakidaiwa kuihusisha Fifa kuamua mechi iendelee.
“Ni fedheha kwa jambo kama hili kutokea na kuitia sumu michezo hii, hali kama hii isingeweza kutokea katika nchi jirani, ni balaa,” aliongeza Mascherano.
Baadaye taarifa kutoka kwa waandaaji yaani Paris 2024 ilieleza kuwa mechi ya Argentina na Morocco kwenye Uwanja wa Saint-Etienne ilisimamishwa baada ya kikundi kidogo cha mashabiki kuvamia uwanjani.
“Baadaye mechi iliendelea na kumalizika kwa usalama, Paris 2024 wanafanya kazi na wahusika ili kujua nini chanzo na kujua hatua sahihi za kuchukua,” ilieleza taarifa ya Paris 2024.
