London, England
Klabu kubwa za soka barani Ulaya kwa kushirikiana na umoja wa wachezaji duniani, wanajipanga kuushitaki uongozi wa Fifa kwa madai ya kutumia vibaya mamlaka yake katika usimamizi wa soka.
Mpango huo unashirikisha ligi 39 pamoja na klabu za soka zaidi ya 1,000 kutoka nchi 30 ambazo kwa pamoja zimefikia uamuzi huo kwa kile wanachodai kuwa ni kulinda ustawi wa wachezaji.
Kiini cha uamuzi huo inadaiwa kuwa ni malalamiko yanayoendelea kutolewa na mamlaka za ligi na umoja wa wachezaji kutokana na ongezeko la idadi ya mashindano kwenye kalenda ya soka na jinsi jambo hilo linavyowaathiri wachezaji.
Taarifa ya Chama cha Wanasoka Profesheno (Fifpro) ilieleza kuwa kalenda ya soka kimataifa kwa sasa imevuka mipaka, haina mustakabali mzuri kwa ligi za taifa na hatari kwa afya za wachezaji.
“Uamuzi wa Fifa katika miaka iliyopita umeendelea kunufaisha mashindano na kuangalia faida za kibiashara na kupuuza wajibu wake kama bodi ya usimamizi na kuathiri mikakati ya kiuchumi ya ligi za taifa na ustawi wa wachezaji,” ilifafanua taarifa ya Fifpro.
Taarifa hiyo pia iliwalaumu mabosi wa Fifa kwa kushikilia msimamo wao wa kukataa kuzihusisha mamlaka za ligi za taifa na umoja wa wachezaji katika taratibu zake za kufanya maamuzi.
Fifa hata hivyo ilijibu madai hayo kwa kuzituhumu baadhi ya ligi kwa unafiki na kusisitiza kwamba kalenda ya Fifa hupitishwa na baraza la shirikisho hilo ambalo linahusisha wajumbe kutoka kila nchi zikiwamo nchi za Ulaya.
Uamuzi wa kuifikisha Fifa mahakamani unatajwa kuwa ni mpango wa pili wenye lengo la kutikisa mamlaka za shirikisho hilo baada ya ule wa kwanza wa baadhi ya klabu barani Ulaya kutaka kuanzisha Super Ligi kufeli.
Rais wa Fifa, Gianni Infantino alinukuliwa akilalamikia uamuzi wa klabu za Ulaya kutaka kuanzisha Super Ligi kwa lengo la kujitenga na Fifa kuwa ni mkakati ambao haukuwa na nia njema na mendeleo ya soka.
