Na mwandishi wetu
Mehboob Manji ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mwenyekiti na mfadhili wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji (pichani) amesema baba yake ambaye alifariki dunia hivi karibuni nchini Marekani, alikuwa Yanga damu.
Akizungumza Jumapili hii katika dua maalum ya kumuombea baba yake, Mehboob alisema mara nyingi Yanga ilipofanya vibaya mzazi wake huyo alikosa raha jambo ambalo liliwafanya yeye na ndugu yake kukaa naye mbali.
Alisema kwamba baba yake aliipenda timu hiyo kwa moyo wake wote na aliposema kaacha moyo wake Jangwani alimaanisha na Yanga iliposhindwa alikuwa akichukia sana.
Mehboob alisema yeye na mdogo wake kuna wakati walikuwa hawahitaji kwenda kuangalia mechi za Yanga ili kujua matokeo badala yake walijua kwa kuangalia sura ya baba yao.
Alisema wakiona amekasirika wanajua Yanga imeshindwa na wakiona ana furaha wanajua Yanga imeshinda na kuna wakati wakiwa nyumbani walilazimika kukaa naye mbali pale matokeo ya Yanga yanapokuwa mabaya.
Mtoto huyo wa Manji ambaye alizungumza kwa Kiswahili kisichofasaha aliwashukuru wale wote walioguswa na msiba huo kwa namna walivyowafariji katika kipindi kigumu mno kwao pamoja na dua walizomuombea baba yao.
Aliwataka radhi watu wa Yanga kwa kumzika baba yake mbali yaani nchini Marekani lakini alisema iliwalazimu kufanya hivyo kwa kuwa mama yake alikuwa huko na alihitaji kuombewa dua na mama yake jambo ambalo ni zuri.
Alisema kwamba baba yake alikuwa mpambanaji na mwenye kupenda kujitolea kwa kutoa misaada kwa watu wenye mahitaji ambao alipenda kuona wanaishi kama binadamu wengine.
Akifafanua kuhusu upambanaji wa baba yake, Mehboob alisema yeye na mdogo wake kuna wakati zilipita siku tatu bila ya kumuona baba yao kwa sababu alilazimika kulala ofisini.
Alisema aliwahi kumuuliza kwa nini alikuwa akifanya hivyo naye alimjibu kwamba akiwa mkubwa atayaona majukumu yalivyo lakini la muhimu alilosisitiza ni kufanya kazi na kuvuka malengo.
Naye Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema kwamba alijuana kwa mara ya kwanza na baba yake Yusuf Manji, Mzee Mehboob Manji wakati akipeleka gari lake kutengenezwa katika gereji yake wakati huo akiwa mtumishi wa chama.
Alisema waliendelea na urafiki wao hata alipokuwa waziri lakini baadaye mzee huyo aliugua saratani na kumwambia kwamba siku zake za kuishi duniani zimebaki chache na kumuusia amtunze kijana wake yaani Yusuf Manji.
Rais huyo mstaafu alisema kwamba alijaribu kumfariji mzee huyo na baadaye alipofariki, mtoto wake yaani Yusuf Manji alipata matatizo na changamoto mbalimbali na yeye alikuwa akimshauri na kumtia moyo.
Soka Mtoto wa Manji: Baba Yanga damu
Mtoto wa Manji: Baba Yanga damu
Read also
