Las Vegas, Marekani
Kocha wa timu ya taifa ya Brazil, Dorival Junior amesema anabeba lawama zote za timu hiyo kutolewa na Uruguay kwa mikwaju ya penalti 4-2 katika mechi ya robo fainali ya Copa America jana Jumamosi.
Uruguay iliyolazimika kucheza na wacheza 10 uwanjani kwa takriban dakika 25 baada ya Nahitan Nandez kupewa kadi nyekundu lakini ilifanikiwa kulazimisha sare ya 0-0 na hatimaye kwenda kwenye mikwaju ya penalti.
“Kazi ya aina hii inahitaji kiwango cha juu cha uvumilivu, najua kwamba haya si matekeo ambayo yalitarajiwa, na hivyo nawajibika kwa lawama zote lakini pia nadhani timu hii ina nafasi kubwa ya kukua na kuwa bora zaidi,” alisema Dorival.
Katika penalti, Douglas Luiz na Eder Militao walishindwa kuifungia Brazil ambayo ilicheza bila ya mshambuliaji wake nyota, Vinicius Junior anayetumikia adhabu wakati kwa Uruguay aliyekosa ni Jose Marta Gimenez.
Uruguay sasa imefuzu nusu fainali ambapo Jumatano ijayo itaikabili Colombia wakati Brazil ikiaga fainali hizo kwa rekodi isiyovutia katika hatua ya makundi baada ya kuambulia ushindi katika mechi moja tu ingawa ilifuzu hatua ya mtoano na hatimaye kukwama mbele ya Uruguay.
“Huu ni kama mchakato, kwa ujumla unapokuwa katika hatua ya kujenga timu unapitia magumu, haya ni mashindano yetu rasmi ya kwanza na matokeo ni ya haki kutokana na kile tulichokitarajia, lengo letu kuu kwa sasa ni kufuzu Kombe la Dunia,” alisema Dorival.
Dorival ambaye tangu akabidhiwe jukumu la kuinoa Brazil hadi sasa ameiongoza katika mechi nane, aliwatetea wachezaji wake akisema wengi wao wameingia katika mashindano hayo baada ya kutoka katika kampeni ngumu na klabu zao.
Kwa Brazil hiki ni kipigo cha pili mfululizo mbele ya Uruguay, Oktoba mwaka jana timu hiyo pia ilifungwa na Uruguay mabao 2-0 katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026.
