Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ameeleza wazi kupiga chini ofa za klabu alizozipata kutokana na majukumu aliyonayo katika kikosi cha Stats.
Morocco ameiambia GreenSports kuwa kwa sasa hatofundisha klabu sambamba na kuinoa Stars kama alivyokuwa akifanya awali kwani kuna kitu anataka kukivuna akiwa na timu hiyo hivyo ameamua kuwekeza huko jumla.
“Ofa zimekuja za hapa Tanzania nyingi tu na chache nje ya nchi lakini nimeamua kuachana nazo sababu kuna kitu nataka kufanya nikiwa na Stars, nataka akili yangu iwe huku kwanza,” alisema Morocco.
Kocha huyo amekuwa akiitumikia Stars huku akizinoa baadhi ya klabu za Ligi Kuu kwa misimu kadhaa kabla ya mwishoni mwa msimu wa 2023-24 kuondoka Geita Gold.
Akizungumzia nafasi ya Taifa Stars katika Kundi H kwenye mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025, alisema nafasi ipo akifafanua mambo kadhaa.
“Kwanza tuna nafasi ya kufuzu kutokana na hamasa na ukuaji wa kiwango wa kikosi chetu, lakini ni muhimu kutokana na uandaaji wetu wa Afcon 2027, lazima tuendelee kuwemo ili ikifika kwetu tuwe tayari kujipigania nyumbani.
“Na makundi yote ni magumu kimsingi, yote yana changamoto lakini tunapaswa kupambana, kujiandaa vya kutosha, kuwa tayari na kuipigania timu na taifa kuipeleka tena Afcon nyingine,” alisema Morocco.
Katika kundi hilo Stars iliyoshiriki michuano hiyo mwaka 1980, 2019 na 2023 itapambana dhidi ya Guinea, DR Congo na Ethiopia katika kuwania nafasi ya timu mbili zitakazofuzu.
