Hamburg, Ujerumani
Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe amesema ni heshima kwake kucheza dhidi ya Cristiano Ronaldo katika mechi ya robo fainali ya Euro 2024 itakayopigwa leo Ijumaa.
Mbappe, 25, nyota wa zamani wa PSG na ambaye tayari ameshasaini kuichezea Real Madrid, timu ambayo Ronaldo ameichezea kwa mafanikio na kushinda mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akiizungumzia mechi hiyo, Mbappe alisema kwamba ni jambo la kufurahia kucheza dhidi ya mchezaji huyo ambaye pia ametwaa tuzo za Ballon d’Or mara tano.
“Kwa wakati wote ni mchezaji ambaye nimekuwa nikivutiwa naye, nimewahi pia kupata nafasi ya kujuana naye na kuzungumza mara kadhaa, huwa tunawasiliana,” alisema Mbappe.
“Wakati wote amekuwa akijaribu kunipa ushauri na kuniarifu mambo mbalimbali yanayoendelea, kucheza dhidi yake ni heshima kutokana na kila kitu ambacho amewahi kukifanya katika soka,” alisema Mbappe.
“Bila ya kujali nini kitatokea kabla au baada ya mchezo, Ronaldo wakati wote atabaki kuwa gwiji lakini mwisho wa yote matumaini yetu Ufaransa ni kushinda na kufikia hatua ya nusu fainali,” alisema Mbappe.
Mbappe pia alisema kwamba Ronaldo ataendelea kuwa mmoja tu na anajiona mwenye bahati kwa kupata fursa ya kuendelea kuzipigania ndoto zake akiwa mchezaji wa Real Madrid kama ilivyokuwa kwa Ronaldo.
Ronaldo, 39, ameshasema kwamba anaamini fainali hizi za Euro 2024 ni za mwisho kwake na haamini kama atashiriki michuano hiyo kwa siku zijazo na hivyo mechi ya leo kwa mujibu wa Mbappe ni kama tukio la wachezaji mahiri kuagana.
Naye kiungo wa Man City, Bernando Silva ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Ureno na aliwahi kuwa pamoja na Mbappe katika timu ya Monaco amesema Mbappe wakati wote ni bora kwenye kundi la wachezaji.

“Kylian ni mchezaji wa kipekee na alianza nasi pale AS Monaco wakati huo akiwa na miaka 16, nakumbuka baada ya wiki ya kwanza tu tulianza kuulizana dogoo huy ni nani,” alisema Silva.
Silva aliwasifia Ronaldo na Mbappe kwa umahiri lakini alikataa kuingia katika hoja ya wachezaji hao kwenye mechi ya leo badala yake alisema kwamba ni mechi inayozihusu Ufaransa na Ureno na si Ronaldo na Mbappe. Mechi ya Ufaransa na Ureno itatanguliwa na mechi nyingine ya robo fainali kati ya wenyeji Ujerumani dhidi ya Hispania.
