Munich, Ujerumani
Beki wa kushoto wa timu ya taifa ya Ureno, Nuno Mendes (pichani) ameelezea furaha na shauku aliyonayo kukutana na mshambuliaji nyota wa Ufaransa, Kylian Mbappe katika mechi ya robo fainali ya Euro 2024 kesho Ijumaa.
Mendes. 22, pia amewahi amecheza na Mbappe misimi miwili katika kikosi cha PSG kabla ya Mbappe kutangaza kuhamia Real Madrid akiwa mchezaji huru hivi karibuni.
Alisema kwamba yuko tayari kukabiliana na Mbappe kama mchezaji huyo atakuwa kwenye eneo lake kwani wakati wote huwa anafanya mazoezi ya kukabiliana na watu wa aina hiyo.
“Sina hakika kama atacheza katika eneo langu lakini kama itatokea hivyo nimeshajiandaa, huwa nafanya mazoezi mara kwa mara kwa matukio haya, tuko tayari kukabiliana nao,” alisema Mendes.
Mendes pia alikiri Ufaransa ina wachezaji wa hadhi ya juu lakini hapo hapo akasisitiza hata wao Ureno wana wachezaji wa aina hiyo na wanahitaji kufanya kila liwezekanalo ili kuizuia nguvu ya Ufaransa ili wao Ureno wacheze soka lao.
Katika kikosi cha Ureno kwenye fainali za Euro 2024 zinazoendelea nchini Ujerumani, Mendes pia yuko timu moja na Cristiano Ronaldo, staa wa zamani wa timu za Man United na Real Madrid na mshindi mara tano wa tuzo za Ballon d’Or.
Akiwazungumzia Mbappe na Ronaldo, Mendes alisema ni wachezaji wa kiwango cha juu duniani wenye uwezo wa kubadili matokeo katika mazingira yoyote.

“Wote hawa nimekuwa nao pamoja kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na ni jambo la kufurahia kucheza na Mbappé na Cristiano. Ni wachezaji wa kipekee, kutoka tukio moja hadi jingine wana uwezo wa kuleta utofauti,” alisema Mendes.
Alipoulizwa kati ya wachezaji hao anaweza kumchagua yupi, Mendes alisema kwamba hilo kwake ni swali gumu na kama angekuwa kocha basi angewachagua wote wawili.
