Na mwandishi wetu
Beki wa kulia wa timu ya PSG ya Ufaransa, Achraf Hakimi ameeleza kwamba haitakuwa mara ya mwisho kuja Tanzania na kutoa misaada kwani ataendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali nchini.
Hakimi raia wa Morocco amezungumza hayo alipokuwa kwenye mchakato wa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali Alhamisi hii katika Shule ya Sekondari ya Patandi mkoani Arusha.
“Niliwahi kuwa hapa katika kucheza mpira, lakini ni mara ya kwanza kuja kufurahia mapumziko yangu, na hii ni mara ya kwanza ‘foundation’ yangu inafanya kazi nje na imekuwa hapa Tanzania.
“Nashukuru kutimia kwa mpango huu kupitia wizara na watendaji wake na mkurugenzi wa shule hapa, asanteni sana, na pia kaka yangu Hersi (Said, Rais wa Yanga SC) ambaye tumefahamiana kwa muda na kuja Tanzania kufanya hivi haitakuwa mara ya mwisho kwa mapenzi niliyonayo moyoni mwangu,” alisema Hakimi mchezaji bora wa PSG msimu wa 2023-24.
Achraf Hakimi Foundation imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh bilioni moja, kuwasaidia wanafunzi zaidi 400 shuleni hapo.
Taasisi hiyo imetoa msaada wa kompyuta 50 kwa ajili ya wanafunzi, kompyuta tano za walimu, samani, mashine za kuchapishia kwa ajili ya wanafunzi wasioona.
Msaada mwingine ni wa ujenzi wa mashine ya kuchemshia maji kwa ajili ya kuchomea nepi, ujenzi wa vyumba viwili vya kompyuta na projector 10.
Hakimi yupo Tanzania tangu Jumatatu ya wiki hii ambapo amekuja kwa ajili ya kufanya utalii kwenye vivutio mbalimbali nchini, akipokelewa na mwenyeji wake, Hersi.
Kimataifa Hakimi aahidi kuja tena Tanzania
Hakimi aahidi kuja tena Tanzania
Read also
