Na mwandishi wetu
Klabu ya Coastal Union inajipanga kufanya usajili wa wachezaji takriban watano kuelekea msimu ujao wa 2024-25 ili kuendelea kuleta hali ya utulivu na umakini kikosini.
Wagosi Wakaya hao wameeleza hayo leo Jumanne kuwa usajili huo utalenga wachezaji wenye wasifu wa kupita kwenye timu zilizoshiriki michuano ya Shirikisho la Soka Afrika ili kuongeza tija.
“Kuna majina takriban ya wachezaji wachache sana ambao tutawasajili na yote kwa yote ni kwa sababu hatutaki tuingize maingizo mengi ili kujenga kwa umakini kikosi chetu kuelekea msimu ujao,” alisema ofisa habari wa Coastal, Abbas El Sabri.
“Ubora na uzuri wa kikosi chetu tayari umeshajionesha tupo vizuri eneo gani, na tuko dhaifu eneo gani kwa hiyo tutakayofanyia kazi ni maeneo machache sana na kusajili wachezaji watano ambao kwanza lazima wawe na uzoefu wa michuano ya Caf,” alieleza Sabri.
Alifafanua kuwa kutafuta ubora wa wachezaji hao ndiko kunakowachelewesha kuweka wazi usajili mpya kwani mchakato wa kunasa wachezaji wazuri wenye wasifu kama huo huwa mgumu kidogo.
Coastal na Simba zitawakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika wakati Yanga na Azam zitapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao wa 2024-25.
