Munich, Ujerumani
Nahodha wa timu ya taifa ya Croatia, Luka Modric amesema ataendelea kuichezea timu hiyo licha ya kuwa na matarajio madogo ya kufuzu hatua ya mtoano ya fainali za Euro 2024 baada ya sare ya bao 1-1 na Italia.
Matokeo hayo ya mechi hiyo ya Kundi B iliyopigwa jana Jumatatu yamewaumiza Croatia ambao walikuwa wa kwanza kupata bao kabla ya Italia kusawazisha na kuifanya timu hiyo ishike nafasi ya tatu katika kundi hilo ikiwa na pointi mbili.
Kwa hali ilivyo pointi hizo ni chache mno kuiwezesha timu hiyo kupata nafasi kati ya timu nne bora zinazomaliza nafasi ya tatu kwa kila kundi na hivyo haitoshangaza Croatia ikiaga fainali hizo zinazoendelea nchini Ujerumani.
Mazingira hayo hata hivyo hayajamkatisha tamaa Modric mwenye umri wa miaka 38 huku akiwa anashikilia rekodi ya mchezaji mwenye umri mkubwa kufunga bao katika fainali hizo.
Modric ambaye alianza kuichezea timu ya taifa ya Croatia mwaka 2006 hadi sasa ana rekodi ya kuichezea timu hiyo mara 178.
“Nitaendelea kuichezea timu hii siku zote ingawa ni wazi kwamba kuna siku itafika ambayo ni lazima nistaafu, lakini kimsingi nitaendelea kucheza na sijui ni hadi lini,” alisema Modric.
Modric alisema ni bahati mbaya matokeo ya mechi yao na Italia yamekuwa ya kikatili kwao licha ya kupambana ni kama ilivyokuwa mechi yao na Albania ambayo waliongoza lakini wapinzani wao wakasawazisha bao dakika za mwisho na matokeo kuwa 2-2.
