Na mwandishi wetu
Timu ya Tanzania Prisons ya Mbeya imemtangaza Mbwana Makata kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo na kurejea katika kikosi hicho kwa mara ya tatu sasa.
Makata anarejea Prisons ikiwa ni wiki moja imepita tangu afungashiwe virago na Pamba Jiji ya Mwanza aliyoipandisha kushiriki Ligi Kuu NBC msimu ujao na mikoba yake kurithiwa na Mserbia, Goran Kopunovic.
Makata amewahi kuinoa Prisons mwaka 2009 kwa msimu mmoja na nusu kabla ya kutimka na kurejea tena mwaka 2015 kurithi mikoba ya marehemu David Mwamwaja.
Akiwa na timu hiyo Makata aliiokoa na janga la kushuka daraja kwa ushindi wa mechi tatu, sare tatu, akipoteza mmoja na kuibuka kocha bora wa ligi kuu msimu huo.
Makata ambaye enzi zake za soka la ushindani alikuwa kipa na aliwahi kudakia timu ya Yanga, pia amewahi kuzinoa timu za Toto Africans, Oljoro JKT, Kagera Sugar na nyinginezo.
Kwa upande wa Prisons anachukua nafasi ya Hamad Ally ambaye zipo habari kwamba yuko njiani kuelekea JKT Tanzania kurithi nafasi ya Malale Hamsini.
Makata aliiongoza vyema Pamba msimu wa 2023-24 kwenye mechi 30 ambapo ilishinda mechi 20, sare saba, ikifungwa mechi tatu na kuvuna pointi 67 zilizowahitimisha kwenye nafasi ya pili ya Ligi ya Championship.
Mbali na Pamba, Makata amewahi pia kuzipandisha daraja timu za Alliance msimu wa 2017-18, Polisi Tanzania (2018-19) na Dodoma Jiji (2019-20).
Soka Makata arejeshwa Prisons
Makata arejeshwa Prisons
Read also
