Leipzig, Ujerumani
Hofu ya mashabiki wa Ufaransa kumkosa mshambuliaji wao tegemeo Kylian Mbappe katika mechi ya leo Ijumaa dhidi ya Uholanzi imefutika baada ya kocha wa timu hiyo, Didier Deschamps kusema kuwa anaamini mchezaji huyo atakuwa fiti.
Mbappe aliumia pua na kushindwa kumaliza dakika zote 90 katika mechi ya kwanza ya Ufaransa dhidi ya Austria iliyoisha kwa Ufaransa kutoka uwanjani na ushindi mwembamba wa bao 1-0.
Mchezaji huyo aliumia wakati akiwania mpira wa juu na beki wa Austria, Kevin Danso katika tukio ambalo baadaye jezi ya Mbappe ilionekana ikiwa na damu na hivyo kutoa dalili kwamba huenda asingeweza kuendelea tena na fainali hizo.
Deschamps hata hivyo aliwahakikishia mashabiki wa Ufaransa walioingia hofu kuwa watafanya kila linalowezekana kuhakikisha mchezaji huyo anakuwa vizuri kwa mechi ya Ijumaa.
“Kila kitu kinakwenda vizuri, baada ya mshtuko tuliokuwa nao, hatimaye (Mbappe) ameweza kufanya mazoezi mepesi (Alhamisi asubuhi) na itakuwa hivyo hivyo jioni, kila kitu kipo katika mwelekeo mzuri,” alisema Deschamps.
Akiwa katika mazoezi na timu ya Ufaransa, Mbappe alionekana akiwa na plasta maalum ya kuzuia sehemu ya pua iliyoumia na inadaiwa huenda akacheza mechi na Uholanzi akiwa na plasta hiyo.
Kupitia mtandao wa Instagram, Mbappe alizidi kuwapa matumaini mashabiki wa Ufaransa kwa andiko lake ambapo alisisitiza nia ya kujitoa kwa namna yoyote bila kuhofia hatari inayoweza kujitokeza kwani tofauti na hivyo ushindi hauwezi kupatikana.
