Manchester, England
Bilionea na mmiliki mwenza wa klabu ya Manchester United, Sir Jim Ratcliffe (pichani) amesema hadhani suluhisho la klabu hiyo linaweza kupatikana kwa kumsajili Kylian Mbappe badala yake ni kuhakikisha wanakuwa na kikosi kilichokamilika kila idara.
Mapema mwezi huu, Real Madrid ilitangaza matarajio yake ya kumsajili Mbappe akiwa mchezaji huru baada ya kumuwinda kwa muda mrefu na zipo habari za ndani kwamba tayari mshambuliaji huyo ameshasaini mkataba na timu hiyo.
Wakati vuguvugu la usajili wa Mbappe likipamba moto baada ya mshambuliaji huyo kutangaza kuwa angeachana na klabu ya PSG baada ya msimu wa 2023-24, Man United nayo iliwahi kutajwa kati ya klabu zilizohitaji huduma yake.
Ratcliffe hata hivyo alisema kwamba hadhani kama suluhisho ni kumnunua Mbappe akisisitiza kwamba mchezaji mmoja kamwe hawezi kumaliza tatizo la Manchester United.
“Jambo la kwanza tunalotakiwa kulifanya ni kutengeneza kikosi kilichokamili, na baada ya hapo labda kuongeza zaidi wachezaji wawili wa hadhi ya Mbappe, itachukua misimu miwili au mitatu kujiweka sehemu nzuri,” alisema Ratcliffe.
Akiizungumzia Real Madrid na mafanikio yake, Ratcliffe aliwataja wachezaji sita wa timu hiyo ambao thamani yake inaweza walau kufikia Dola 100 milioni ambao ni Jude Bellingham, Eduardo Camavinga, VinÃcius Júnior, Federico Valverde, Rodrygo na Aurélien Tchouaméni.
“Kama utaangalia vikosi vya Man United na Real Madrid utaona Real Madrid wana wachezaji sita ambao thamani yao ni zaidi ya Dola milioni 100, Man United haina wachezaji ambao thamani yao ni zaidi ya Dola 70 milioni,” alisema Ratcliffe.
