Stuttgart, Ujerumani
Ushindi wa mabao 5-1 ambao Ujerumani iliupata dhidi ya Scotland umempa kiburi kocha wa timu hiyo, Julian Nagelsmann ambaye sasa anaamini timu yake ina uwezo wa kufanya hivyo tena katika mechi na Hungary.
Ujerumani, wenyeji wa fainali za soka za Euro 2024 zinazoendelea nchini humo leo Jumatano wataumana na Hungary katika mechi yao ya pili ya michuano hiyo.
Nagelsmann hata hivyo pamoja na kujiamini ameonesha kuihofia Hungary kwamba inaweza kuwa tishio hapo hapo akadai kwamba timu hiyo anavyoiona ni kama ipo kiwango sawa na Scotland.
Nagelsmann alisema Hungary ni timu ambayo inacheza soka linalobadilika na huwa haijalishi aina ya mshambuliaji wanayekuwa naye, ni hatari kwa kutengeneza mashambulizi lakini amewaandaa wachezaji wake na kila kitu kitaonekana uwanjani.
“Labda watalazimika kucheza soka la kushambulia kidogo kwa sababu vinginevyo wanaweza kutolewa kwenye mashindano ingawa matarajio yetu ni kucheza vile vile kama tulivyocheza dhidi ya Scotland,” alisema Nagelsmann.
Nagelsmann, kocha wa zamani wa timu za RB Leipzig, Hoffenheim na Bayern Munich anapajua vizuri Stuttgart akiwa katika mechi za Bundesliga na anaamini mashabiki wa mji huo watakuwa vizuri kwa timu yake.
Beki wa Ujerumani, Maximilian Mittelstadt ambaye pia ni mchezaji wa klabu ya FC Stuttgart yuko tayari kucheza katika dimba la nyumbani lakini anatambua kwamba mechi haiwezi kuwa rahisi.
