Munich, Ujerumani
Bao pekee la Jude Bellingham dhidi ya Serbia limetosha kuibeba England kwenye fainali za soka za Euro 2024 zinazoendelea nchini Ujerumani ingawa kiwango cha timu hiyo kimeanza kuibua wasiwasi.
Katika mechi hiyo iliyopigwa jana Jumapili, Bellingham nyota wa Real Madrid alifunga bao hilo pekee katika dakika ya 13 kwa kichwa akiunganisha krosi iliyoanzia kwa Bukayo Saka.
Mashabiki wa England walimshangilia mara kwa mara Bellingham ambaye alionekana kuwa shujaa wao kwa kuwapa bao ambalo limewawezesha kushika usukani Kundi C ambalo pia lina timu za Denmark na Slovenia zilizotoka sare ya bao 1-1 jana hiyo hiyo.
Bellingham ndiye aliyeanzisha shambulizi lililozaa bao hilo na kwa kiasi kikubwa ndiye aliyekuwa kinara wa mashambulizi ya timu hiyo na haikushangaza kwa mashabiki kumshangilia kwa kumtaja jina lake mara kwa mara.
Pamoja na ushindi huo, bado kiwango cha England kimeacha maswali kama ni timu ambayo itaweza kufika mbali au hata kubeba taji hilo hasa kwa kuwa ilikuwa ikitajwa kati ya timu zenye uwezo huo.
Bellingham hata hivyo hakubaliani na mtazamo wa England imecheza kiwango duni badala yake anaamini timu hiyo imeonesha uwezo na ndio maana imetoka na ushindi.
“Sikubaliani na hilo, nafikiri kipindi cha kwanza tumeonesha jinsi tunavyoweza kufunga goli dhidi ya timu yoyote na kipindi cha pili tumeonesha ni kwa nini tuna uwezo wa kuzuia tusifungwe na timu yoyote,” alisema Bellingham.
Nahodha na mshambuliaji tegemeo wa England, Harry Kane alisema kwamba japo kiwango hakikuwa kizuri lakini jambo zuri ni kwamba wamepata ushindi muhimu.
“Kwa ujumla ni ushindi tuliostahili, ni suala la kupiga hatua, kuna wakati kipindi cha pili tulijikuta tukirundikana katika eneo letu na tulipata tabu kidogo kutoka, yote kwa yote huu ni ushindi muhimu,” alisema Kane.
