Na mwandishi wetu
Mshambuliaji George Mpole amesema ingawa amemalizana na FC Lupopo ya DR Congo lakini tayari ana ofa lukuki kutoka nje ya nchi na anahitaji muda kufanya maamuzi.
Mpole ambaye ametua Tanzania jana Ijumaa ameeleza hayo leo Jumamosi jijini Dar es Salaam akifafanua kuwa bado hajakutana na ofa ya timu za Tanzania hadi sasa lakini za nje zipo za kutosha.
“Nina ofa nyingi nje ya nchi ambazo tumepigiwa simu kwa hiyo nimerudi kwanza nyumbani, nipo kwenye mapumziko lakini tutakaa na uongozi wangu tuone kama tunaweza kuzifanyia kazi.
“Tunapaswa kuangalia zaidi wapi ni sehemu bora kwangu, ligi gani ni nzuri kwetu na ambayo tutaendelea kunufaika na kupata muendelezo mzuri zaidi kiushindani wa soka ila kwa Tanzania ndio kwanza nimefika, bado sijafahamu lolote kuhusu ofa,” alisema Mpole.
Mpole aliyeibuka mfungaji bora msimu wa 2021-22 wa ligi kuu baada ya kufunga mabao 17 akiwa na Geita Gold kisha msimu uliofuata alitimkia Lupopo.
Akiwa Lupopo alisaini mkataba wa miaka miwili ambao umemalizika huku akiweka wazi kuwa hana mpango wa kuendelea kukipiga katika timu hiyo.
