Na mwandishi wetu
Maandalizi ya msimu ujao kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga yameanza mapema baada ya kuanza kufumuliwa kwa ‘pitch’ ya uwanja huo ikiwa ni hatua ya awali ya ukarabati wake ili kuufanya uwe bora.
Uwanja huo unaotumiwa na Coastal Union ambao msimu ujao watashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, utawekwa majani yenye hadhi sawa na ya Uwanja wa Mkapa uliopo Dar es Salaam.
“Tayari sisi kama shirikisho (Shirikisho la Soka Tanzania) tumeleta majani, yanakuja na sasa hivi ni maandalizi kwa ajili ya pitch,” alianza kufafanua Rais wa TFF, Wallace Karia.
“Tumeanza kuondoa majani yaliyokuwepo, kuondoa udongo uliokuwepo na watalaamu wetu kesho Jumamosi watakuwepo hapa kueleza ni aina gani ya udongo unaopaswa kuwekwa.
“Na kuonesha jinsi gani yataoteshwa hayo majani ili yaweze kuota na yawe katika kiwango kinachostahili. Majani haya yatakapokuwa yameota itakuwa ni uwanja huu na wa Mkapa ndio utakaokuwa na majani ya aina hiyo, kwa hiyo pitch ya Mkwakwani itakua kama ya Kwa Mkapa,” alisema Karia.
Karia alisema kuwa suala la vyumba na jukwaa kuu, wameshalifanyia utaratibu wa kumleta mchoraji ambaye atawaeleza undani wa michoro hiyo na wao kurekebisha baadhi ya mambo kabla ya kuendelea na ukarabati huo wenye tija pia kwa ajili ya michuano ya klabu Afrika msimu ujao.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Coastal, Hassan Muhsin alisema: “Tumepambana zaidi ya mara tatu kutoshuka daraja lakini tumefurahi mwaka huu Mungu ametusaidia tumepata nafasi ya nne imetupeleka mashindano ya kimataifa.
“Lakini mashindano hayo yanahitaji maandalizi makubwa sana, sasa niwasihi kwamba ule ushirikiano tulioufanya wakati ule uliotupa, sasa safari hii kupitia hii nafasi tunatakiwa kuuzidisha maradufu zaidi ya awali,” alisema Muhsin.
