Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa zamani wa Simba na mdau wa Tabora United, Ismail Aden Rage ameitaka timu ya Tabora kutokata tamaa ya kusalia Ligi Kuu NBC kwani bado wana nafasi ya kufanya hivyo kama wataamka mapema.
Rage ametoa rai hiyo baada ya Tabora kuchezea kipigo cha mabao 4-0 jana Jumanne dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora katika mechi ya awali ya kuwania kubaki ligi kuu msimu ujao. Mechi ya marudiano ni Juni 8, mwaka huu.
“Niwaambie tu Tabora wasikate tamaa bado kuna nafasi ya mechi ya pili ya marudiano, hata kama itaonekana idadi ya mabao ni kubwa na bahati mbaya ikashindikana kupata matokeo mchezo wa pili basi kuna mchezo na Biashara United pia.
“Kwa hiyo bado kuna nafasi nyingine hata kama hii ikipotea, wanaweza kujipanga na kupambana upya na kusalia ligi kuu kupitia Biashara na pia nimezungumza na benchi la ufundi na kuwaeleza makosa machache ya ulinzi ndiyo yametugharimu,” alisema Rage mchezaji wa zamani wa Simba.
Mshindi wa jumla baina ya JKT na Tabora atasalia ligi kuu wakati aliyeshindwa atavaana na Biashara ya Championship kwa ajili ya mechi mbili za mwisho za kutafuta kushiriki ligi kuu msimu ujao wa 2024-25.
