Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amemtaka kiungo wake Toni Kroos kufikiria upya uamuzi wa kustaafu soka baada ya kuisaidia timu hiyo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya 15 ikiichapa Borussia Dortmund mabao 2-0.
Kroos, 34, Jumamosi katika dimba la Wembley alifanikiwa kubeba taji hilo ikiwa ni mara yake ya tano akiwa na jezi ya Real Madrid na mara moja na Bayern Munich.
Mwanzoni mwa msimu huu Kroos alisema kwamba atastaafu soka baada ya kuiwakilisha Ujerumani kwenye fainali za Kombe la Ulaya au Euro 2024 jambo ambalo Ancelotti anaonekana kutolikubali.
Kauli ya Ancelotti hapana shaka imekuja baada ya kumshuhudia Kroos akipika bao la kwanza la Real Madrid katika mechi na Dortmund baada ya kumuunganishia pande Dani Carvajal aliyeujaza mpira wavuni.
“Namshuruku sana Kroos, anamaliza akiwa juu, hakuna namna ya kumaliza ukiwa katika kiwango cha juu kama hivi, ana ujasiri wa kumaliza maisha yake ya soka, na tayari ni mkongwe katika klabu hii,” alisema Ancelotti.
“Mashabiki wote wanamshukuru kwa tabia zake, jinsi alivyokuwa profesheno, na nimeshamwambia kwamba tunamsubiri abadili maamuzi yake, tunakusubiri,” alisema Ancelotti.
Wakati Kroos akijiandaa kuondoka, Real Madrid inatarajia ikamtambulisha rasmi mshambuliaji wao mpya, Kylian Mbappe wakati wowote wiki hii na kuhusu Kroos, Ancelotti amesema wataangalia namna ya kuziba pengo lake kwa kutumia wachezaji waliopo.
