Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismael Aden Rage amewataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuepuka malumbano na kuwa wamoja wakati huu wa kuisuka timu kuelekea msimu ujao.
Rage ameeleza hayo jijini Dar es Salaam akifafanua kuwa kumaliza nafasi ya tatu Simba haimaanishi kuwa haikupambana bali hata ugumu wa Ligi Kuu NBC msimu huu umechangia hali hiyo.
“Nitoe tu ushauri kwa Wanasimba kwamba ‘wasipaniki’, wasigombane na viongozi wao, wamsikilize kocha (kaimu kocha mkuu, Juma Mgunda) ambaye mimi namwamini sana sababu ni kocha mwenye taaluma kubwa kuliko yeyote Tanzania.
“Wawaige wenzetu wa Afrika Magharibi sasa hivi timu zao zenye mafanikio zina makocha wazawa, lakini pia Mgunda anazungumza Kiswahili na Kingereza fasaha kwa hiyo ni mtu sahihi kwa wachezaji na kwenye mawasiliano kwa ujumla,” alisema Rage.
Alisema kutofanikiwa kwenda kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kumaliza nafasi ya tatu haimaanishi wasifanye vizuri msimu ujao kwani wanapaswa kutumia msimu ujao kuamka upya na kudhihirisha Simba ni nani.
Simba ambayo hivi karibuni imekuwa ikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa na kuishia robo fainali, safari hii imeshindwa kufuzu kushiriki michuano hiyo baada ya kumaliza nyuma ya Azam FC walioshika nafasi ya pili na mabingwa wakiwa Yanga.
