Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema anafurahi kuona kikosi chake kikiwa na maandalizi mazuri kuelekea mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Indonesia, Juni 2, mwaka huu.
Stars imetua Indonesia Ijumaa na kufanya mazoezi ya kwanza kwa ajili ya mechi hiyo ambayo ni maandalizi ya kuelekea mechi yao na Zambia itakayochezwa Juni 11, mwaka huu ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Akizungumza kupitia mtandao wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Morocco ameeleza anafurahi na kufarijika kuona wachezaji wanaelewa mapema maelekezo anayowapa wakionesha utayari wa kupigania taifa.
“Ukiachilia wachezaji wote kuwa kwenye afya njema, pia wako tayari kimaelekezo na wanapokea mapema, pia kikosi tulichonacho ni kizuri kwa kuongezea na wale wengine tulioenda Sudan kwa maandalizi na wengine pia wataingia leo usiku (Ijumaa), hivyo mambo yanaendelea kuwa mazuri.
“Hapa tunawakosa wachezaji wa Azam na Yanga ambao nao tutaungana nao timu ikirejea nyumbani lakini tulionao huku wataongeza kuwa fiti na ujuzi tayari kwa kucheza na Indonesia lakini watakuwa vizuri pia mpaka itakapofika wakati wa kucheza na Zambia,” alisema Morocco.
Katika msimamo wa Kundi E la kuwania kufuzu Kombe la Dunia, Stars inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi tatu, sawa na Morocco, Zambia na Niger walio na pointi tatu pia lakini wakitofautiana kwa mabao ya kufunga.
Katika mechi ya kwanza, Stars ilishinda bao 1-0 ugenini dhidi ya Niger kabla ya kuruhusu kipondo cha mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Morocco.
