Cairo, Misri
Timu ya Al Ahly ya Misri ndio wafalme wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023-24 baada ya kuilaza Esperance ya Tunisia bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Jumamosi hii jioni kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
Ushindi huo unaifanya Ahly kuweka rekodi ya kubeba taji hilo kwa mara ya 12 lakini pia unaifanya timu hiyo iwe imebeba taji hilo kubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika kwa mara ya nne katika kipindi cha miaka mitano.
Ushindi huo pia unaifanya Ahly iweke rekodi ya kucheza mechi 20 za ligi hiyo bila kupoteza lakini pia imeweka rekodi ya kuvutia katika safu yake ya ulinzi ikiwa imefungwa bao moja tu kwa msimu huu.
Esperance katika mechi hiyo iliingia na shauku kubwa ya kubeba taji hilo ikiamini ulikuwa wakati wake sahihi kufanya hivyo ikiwania rekodi ya kulibeba kwa mara tano ikikumbukwa kuwa ilifanya hivyo mara ya mwisho mwaka 2019.
Mambo hata hivyo yaliwaharibikia Esperance mapema dakika ya nne baada ya Roger Aholou kujifunga wakati akiokoa mpira wa kichwa uliopigwa na Ramy Moustafa ukitokana na kona iliyochongwa na Hussein El Shahata.
Ahly waliweza kulilinda vyema bao hilo na hadi dakika 90 zinakamilika walitoka vifua mbele wakineemeka pia na matokeo ya awali katika mechi ya kwanza iliyopigwa mjini Tunis na timu hizo kutoka sare ya bila kufungana.
Uwanja wa Kimataifa Cairo ulilipuka kwa shangwe baada ya wafalme hao wa soka la Afrika kumaliza dakika 90 wakiwa mashujaa na rekodi yao ya kubeba taji hilo kwa mara ya 12.
Kimataifa Al Ahly wafalme Ligi ya Mabingwa
Al Ahly wafalme Ligi ya Mabingwa
Read also
