Barcelona, Hispania
Hatimaye klabu ya Barcelona imetangaza rasmi kumfuta kazi kocha Xavi huku kocha wa zamani wa Bayern Munich, Hansi Flick akitarajiwa kuchukua nafasi yake.
Hatua ya kumtimua Xavi imekuja baada ya hivi karibuni kuibuka mjadala juu ya hatma yake hasa baada ya kuwapo madai kwamba klabu hiyo ilipanga kumbakisha licha ya kocha huyo kutangaza Januari mwaka huu kwamba ataondoka baada ya msimu huu.
Xavi, 44, hata hivyo keshokutwa Jumapili atakuwa uwanjani katika mechi ya mwisho ya msimu wa 2023-24 wa La Liga ambapo Barca itakuwa nyumbani ikiumana na Sevilla.
Mkataba wa Xavi na Barca unafikia ukomo mwaka 2025 lakini uamuzi wa kuachana naye umekuja baada ya kikao kati ya rais wa klabu hiyo, Joan Laporta na mkurugenzi wa michezo, Deco ambacho kilifanyika leo Ijumaa.
Habari za Xavi kuendelea kuinoa Barca zilipata nguvu mwezi uliopita lakini inadaiwa aliponzwa na kauli yake alipozungumzia matatizo ya kiuchumi ya Barca akidai itakuwa vigumu kwa timu hiyo kushindana na Real Madrid na klabu nyingine kubwa za Ulaya.
Taarifa ya Barca ilimshukuru Xavi kwa kazi aliyoifanya tangu akabidhiwe majukumu ya kuinoa timu hiyo mwaka 2021 na msimu uliopita wa 2022-23 aliiwezesha kutwaa taji la La Liga.
“Haijawahi kuwa rahisi kuiacha klabu ya maisha yako lakini najivunia miaka miwili na nusu kuwa kiongozi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, hii imekuwa kama familia yangu ya pili,” alisema Xavi.
Xavi alisema baada ya Jumapili atabaki kuwa shabiki wa Barca jukwaani, na hilo halimpi shida kwa sababu kabla ya kuwa mchezaji au kocha yeye ni shabiki wa Barca na amekuwa katika maisha yake yote akiitakia mema klabu hiyo.
Baada ya kutangaza kuachana na Xavi, Barca ilidai kwamba mfumo mpya wa uendeshaji imu hiyo na benchi la ufundi vitawekwa wazi katika siku chache zijazo baada ya Flick kuanza kazi.
Flick, 59 amekuwa bila kazi tangu Septemba 2023 alipotimuliwa Bayern, timu ambayo anajivunia rekodi yake ya mwaka 2020 alipoiwezesha kubeba mataji matatu ya Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga, DFB-Pokal na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
