Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa KMC, John Matambala (pichani) amesema wamejiandaa takriban wiki nzima kwa ajili ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mechi yao ya kesho Jumamosi dhidi ya Simba ili kutimiza ndoto yao ya kumaliza kwenye nne bora.
Matambala ameeleza hayo leo Ijumaa kuelekea mchezo wao huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha akisisitiza kuwa licha ya kubadilishwa kwa uwanja huo dakika za mwisho lakini haijabadili chochote katika azma ya kutafuta matokeo katika mechi hiyo.
“Tumesafiri salama kufika hapa Arusha, maandalizi yako salama na tuko tayari na mchezo wetu wa Simba, maandalizi tumeyafanya zaidi ya wiki nzima sasa, tumepata taarifa ya ghafla kubadilishiwa uwanja na sisi KMC kama wanajeshi baada ya taarifa hiyo tukajipanga haraka tukaja Arusha.
“Mechi ya kwanza na Simba iliisha kwa sare kutokana na kila mmoja kuwa bora upande wake, lakini kiujumla KMC tunauhitaji zaidi mchezo wa kesho kupata pointi maana tunahitaji kupanda juu zaidi, lengo letu ni kumaliza kwenye nne bora, tunafahamu hautakuwa mchezo mwepesi lakini tumejipanga kupambana na Simba,” alisema Matambala.
Naye, kaimu kocha mkuu Simba, Juma Mgunda alisema: “Maandalizi yamekamilika na tumekuja hapa Arusha kutimiza kile tulichokiandaa, hivyo kesho tuko tayari kwa maana ya maandalizi tuliyofanya kwa ajili ya mechi hii muhimu, naamini mechi itakuwa ngumu na ushindani kutokana na mahitaji.
“Sisi tuna mahitaji yetu na wapinzani wana yao, lakini kwa kanuni ya mchezo wa kiungwana lazima umuheshimu mpinzani wako, hivyo tunamheshimu mpinzani wetu lakini niseme maandalizi yote ya kucheza mechi ngumu nzito ya kesho yamekamilika.”
Simba inayoshika nafasi ya tatu kwa pointi 63 sawa na Azam inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga inahitaji kumaliza ya pili ili kuiwakilisha nchi msimu ujao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
KMC inayoshika nafasi ya tano kwa pointi 36 ikijiwinda kuipita Coastal Union inayomiliki nafasi ya nne kwa pointi 41 huku ikisalia mechi na mechi mbili kabla ya ligi kumalizika.
