London, England
Kocha Mauricio Pochettino ameachana na klabu ya Chelsea kwa makubaliano ya pande mbili na tayari zipo habari kwamba anawindwa na klabu za Man United na Bayern Munich.
Pochettino amechukua uamuzi huo ikiwa imepita takriban wiki moja tangu atetewe na mwenyekiti wa klabu hiyo, Todd Boehly ambaye alisema kocha huyo anahitaji kuvumiliwa kwa kuwa mambo yameanza kuwa mazuri na timu imekuwa ikiimarika.
Chelsea ilimuajiri Pochettino Julai Mosi mwaka jana kwa mkataba wa miaka miwili ambao ulikuwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja lakini ameamua kuondoka kabla ya mkataba wake kufikia ukomo.
Kwa kipindi kirefu kocha huyo kutoka Argentina amekuwa na wakati mgumu kwenye kikosi cha Chelsea lakini ushindi wa mechi tano mfululizo ulionekana kubadili upepo na alipongezwa na Boehly baada ya sare moja na kushinda mechi mbili.
Mafanikio ya hivi karibuni yameifikisha Chelsea katika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu England (EPL) lakini pia timu hiyo ilifikia fainali ya Carabao na nusu fainali ya Kombe la FA.
“Asante kwa wamiliki wa Chelsea na wakurugenzi wa michezo kwa fursa mliyonipa, kwa sasa klabu ipo katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye ligi kuu pamoja na Ulaya kwa miaka ijayo,” alisema Pochettino.
Kuondoka kwa Pochettino (52) kunaifanya Chelsea kuanza kusaka kocha wa kuchukua nafasi yake na tayari baadhi ya majina yameanza kutajwa akiwamo kocha wa Ipswich, Kieran McKenna, Ruben Amorin wa Sporting na Vincent Kompany wa Burnley.
Pochettino alikabidhiwa jukumu la kuinoa Chelsea baada ya kutimuliwa kwa makocha kadhaa katika kipindi kisichozidi miaka mitano wakiwamo Thomas Tuchel, Graham Potter na Frank Lampard ambaye alikuwa kocha wa muda mwishoni mwa msimu wa 2022-23.
Kuhusu uwezekano wa Pochettino kwenda Man United au Bayern ambazo zinasaka makocha wapya, habari hizo zimeandikwa na vyanzo mbalimbali vya habari barani Ulaya.
