Na Hassan Kingu
Kwanza tuelewane jambo moja, hakuna timu mbovu inayoweza kufikia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, halafu timu hiyo hiyo mbovu ikatolewa kwa mbinde na Al Ahly ya Misri, timu yenye hadhi na heshima yake Afrika.
Timu mbovu inayoweza kupambana na kuzipiku timu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hadi hatua ya makundi na hatimaye kufuzu robo fainali, hiyo haiwezi kuwa mbovu, ni timu nzuri, yenye wachezaji wazuri lakini inaweza kuwa na matatizo mengine.
Wanaoamini Simba hii mbovu wanataka kutuambia kwamba imebahatisha hadi kufikia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imewatoa vibonde kuanzia mwanzo hadi makundi, kwamba kwenye hatua ya makundi kulikuwa na timu vibonde.
Katika hilo wapo ambao wanaiponda Simba lakini ukiwauliza mbovu kivipi wanaitaja mechi moja ya ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy.
Eti Simba waliifunga Galaxy kwa sababu ilikuwa na wachezaji wazee, wachezaji wenyewe ni wale walioingia kipindi cha pili tena baada ya Galaxy kuona wamezidiwa wakaona wawaingize wakongwe ambao kila timu inao.
Ikumbukwe kuwa hadithi hii ya wachezaji wazee ilianzia kwa mashabiki wa Yanga, wakati Simba wakijivunia ushindi huo, Yanga walikuwa wakiwabeza kwamba wameifungia timu iliyojaa wazee na Simba nao wakingia humo humo.
Ukiachana na hadithi ya Galaxy pia wapo wachezaji Simba ambao wanahusishwa mara kwa mara na ubovu wa timu, hawa ndio wahanga wa Simba inayoitwa mbovu, wamekuwa wakilaumiwa na hata baadhi ya mashabiki na wachambuzi wakitaka Simba iachane nao.
Aishi Manula
Mmoja wa wachezaji hao ni kipa Aishi Manula, huyu tangu afungwe katika mechi dhidi ya Yanga amekuwa akitupiwa lawama za mara kwa mara na kuonekana hana nafasi tena ndani ya Simba.

Ukiniuliza mimi kuhusu Manula nilichokiona ni kwamba tangu aumie hakuwa tena Manula yule wa siku za nyuma, na bahati mbaya sana akakutana na mechi dhidi ya Yanga akiwa katika siku zake za mwanzo mwanzo baada ya kupona.
Manula alihitaji kuangaliwa katika namna nyingine kabisa ili arudi upya na kuwa Manula yule yule aliyezoeleka kwani naamini bado Simba inamhitaji na kwa kuwa tayari yupo Ayoub Lakred na Ally Salim, makipa hao watatu wanatosha kwa sasa, Simba iwaamini.
Shomari Kapombe
Huyu naye ni mhanga wa Simba mbovu, mara kadhaa amejikuta akishushiwa lawama kwa hoja kwamba ameanza kuchoka na hivyo Simba inatakiwa itafute mtu mwingine na huyu iachane naye.

Kwa Kapombe mimi naamini bado ana nafasi Simba ili anahitaji beki mwingine wa hadhi yake kwa lengo la kumpa changamoto na katika Ligi Kuu NBC ninayemuona anafaa kuchukua nafasi ya Kapombe ni Yao Kouasi wa Yanga.
Zaidi ya Yao sijaona beki ambaye unaweza kusema ni mbadala wa Kapombe, tofauti na hivyo Simba wanaweza kujikuta katika matatizo kuliko haya wanayoyaona mara chache kwa Kapombe, na hapa kwa mara nyingine naizungumzia Simba ambayo tayari ina hadhi ya kushindana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika si Ligi Kuu NBC pekee.
Simba iliyofikia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zaidi ya mara moja kama imemchoka Kapombe basi mbadala wa haraka haraka ni Yao, vinginevyo ivunje benki, itoke nje ya nchi. Kumbuka tu naizungumzia Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mohamed Hussein Zimbwe Jr
Huyu si mara kwa mara kusemwa vibaya lakini naye inapotokea kafanya kosa haraka haraka akili ya mashabiki inajiaminisha kwamba amechoka eti kwa sababu ameichezea Simba kwa muda mrefu hivyo ni wakati wake wa kuondoka.

Kama kuna kosa ambalo Simba inaweza kulifanya basi kosa hilo litakuwa kuachana na Zimbwe Jr, ikimuacha tu itamuona mtaa wa pili au wa tatu tena baada ya siku chache.
Wanaodhani kwamba Zimbwe Jr amefikia mwisho wakumbuke kwamba duniani na si Tanzania tu, wachezaji wanaomudu kuitumia vyema miguu ya kushoto ni wachache na kwa hapa Tanzania beki anayemudu kuutumia vyema mguu huo kwa sasa ni Zimbwe Jr.
Nikimuona Zimbwe Jr nakumbuka jinsi Kenny Mkapa alivyodumu katika nafasi ya kushoto akiwa na timu ya Yanga, miaka nenda rudi, panga pangua Kenny alikuwa hakosekani shavu la kushoto, wenye rekodi zao wanalijua hili vyema.
Sikatai Zimbwe amecheza Simba kwa muda mrefu na ana mapungufu ya hapa na pale lakini sikubali kwamba Simba inatakiwa japo kufikiria kuachana naye, Zimbwe naye anahitaji mtu wa kumpa changamoto na hiyo ndiyo hali halisi ya kila jambo.
Na kama kuna ulazima wa kuachana na Zimbwe Jr basi wanaoamini hivyo wamtaje beki wa hapa Bongo ambaye wanadhani anaweza kuchukua nafasi yake na kukawa na mabadiliko ya kiuchezaji kwenye timu, na awe beki wa hadhi ya Ligi ya Mabingwa Afrika si Ligi Kuu NBC pekee.
Nasema hivyo kwa sababu haitoshi kuishia kusema hafai bila kutaja mtu sahihi ambaye anaweza kuchukua nafasi ya huyo asiyefaa, nadhani anayetaja mbadala anakuwa pia ameonesha dhamira njema ya kuisaidia timu.
Henock Inonga
Kwa Inonga naye naamini bado anahitajika Simba ingawa tatizo kubwa la kuwa majeruhi mara kadhaa limekuwa likimtoa katika ubora wake lakini naye anabaki kuwa mtu muhimu wa Simba ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kama dhamira ya Simba ni kwenda nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa basi Inonga naye anapaswa kuwamo katika hesabu hizo ingawa wakati mwingine nadhani apewe muda awe amepona na kuwa fiti kwa asilimia 100.
Ninachokiona kwake ni kama vile anawahishwa au anajiwahisha kuingia uwanjani kabla hajapona na ndio maana kuna wakati akiguswa kidogo tu anarudi pale pale na kuwa mchezaji majeruhi.
Na kama kuna anayedhani Inonga amefikia mwisho na anatakiwa kuondoka Simba basi kwangu mtu sahihi wa kuchukua nafasi hiyo ni Ibrahim Bacca wa Yanga, kama Simba itafanya hivyo itakuwa imetoa jembe imeingiza jembe au itafute beki sahihi wa kuziba nafasi yake ikiwezekana nje ya nchi.
Angalizo tu, mtazamo uwe ni ushiriki wa timu ya Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kufikia hatua ya nusu fainali isiwe ni mtazamo wa Ligi Kuu NBC au Kombe la Shirikisho CRDB pekee.
Simba hii imecheza sana robo fainali Ligi ya Mabingwa, mawazo sasa yawe nusu fainali au hata fainali na wachezaji ni lazima wasajiliwe kwa mtazamo huo.
Che Malone
Kwangu huyu namuona ni beki mzuri, ameonesha mara kadhaa uimara wake ingawa naye kuna wakati amekuwa akitajwa tajwa japo si sana lakini kwangu naamini Simba haina sababu ya kuachana naye.

Ukiacha uwezo wake wa kukaba na wakati mwingine kuufanya mpira uwe burudani, Che Malone ni beki mwenye kujiamini sifa ambayo inahitajika, amedhihirisha hilo mara kadhaa na anakumbukwa siku ambayo aliingia katika ugomvi na kipa wake, Ally Salim tatizo likiwa ni kujiamini kulikopitiliza kwa Che Malone.
Kwa walioangalia vizuri tukio hilo, Che Malone kwa kumuangalia usoni alikuwa amejiridhisha kuwa mpira ulishafika kwenye himaya ya Ally Salim au ulikuwa lazima ufike kwenye himaya ya kipa huyo lakini kipa huyo akaingia hofu na kumlaumu Che Malone na wawili hao kujikuta katika mzozo.
Kilichotokea kwa wawili hao ni beki mwenye kujiamini na aliyekiamini alichokifanya na kipa ambaye alitawaliwa na hofu.
Clatous Chota Chama
Mhanga Mwingine wa Simba ni kiungo Clatous Chama, kwa Chama kama walivyo hao wengine naamini Simba ikiamua kuachana naye leo, kesho itamuona mtaa wa pili.

Chama kwangu naona ni aina ya mchezaji ambaye unaweza kumhitaji hasa timu inapokuwa katika mazingira magumu ya kusaka bao la ushindi au la kusawazisha hasa katika dakika za lala salama, ana uwezo wa kufungua timu, kumiliki mpira, kupiga chenga mbili tatu na kutoa pasi za maana.
Anajua kuufanya mpira uwe burudani, ni wachezaji wachache mno kwenye ligi ya Tanzania wenye ujasiri wa Chama ambaye wakati mwingine anajikuta akicheza rafu za hovyo pale anapoitafutia timu yake bao hasa dakika za lala salama.
Chama ni kiwango sahihi cha Simba inayosaka mafanikio kwenye Ligi ya Mabingwa, na pengine ndio maana amekuwa chaguo kwa makocha wote wa kigeni waliokuwa Simba akiwamo Abdelhak Benchikha.
Kitu pekee ambacho nakiona kwa Chama ni ukweli kwamba si mchezaji wa dakika 90, kocha akijua kumtumia vizuri Chama timu inaweza kufaidika naye, si mchezaji wa kuachwa.
Saido Ntibazonkiza
Ntibazonkiza naye ni hivyo hivyo, ubora wake ndio uliowafanya Simba wamchukue haraka kutoka Geita Gold baada ya kuachwa na Yanga kiasi kwamba baadhi ya mashabiki walifikia hatua ya kujenga hisia kwamba kuondoka kwake Yanga haikuwa bure, bali kuna namna ilitumika.

Ntibazonkiza baada tu ya kutua Simba moja kwa moja akaenda kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu NBC msimu uliopita, jambo ambalo lilidhihirisha kwamba Simba ilifanya uamuzi sahihi kumchukua kutoka Geita.
Sifa ambayo ameionesha Ntibazonkiza ni kama ya Chama, uwezo wa kumiliki mpira, kupiga chenga na kutafuta bao wakati timu inapokuwa kwenye mazingira magumu ya kusaka ushindi au sare wakati muda ukienda.
Kwa Ntibazonkiza hata hivyo kama ilivyo kwa Chama naye si mchezaji wa dakika 90, lakini hilo kwangu halitoshi kumfanya aonekane hafai Simba, badala yake Simba inahitaji mchezaji wa aina yake hasa kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kuna shabiki alisikika akisema kwamba Chama na Ntibazonkizao wamechoka na kusema kwamba wanakimbia kichovu kwa kujivuta, huyu bila shaka atakuwa anazungumzia wanapotolewa uwanjani ili aingizwe mchezaji mwingine baada ya timu yao kupata ushindi na wao kutoka kwa staili ya kupoteza muda.
Matatizo matatu Simba
Kwa nionavyo Simba hii ina matatizo matatu, moja haina mshambuliaji kwa maana ya mtu ambaye anaweza kuaminiwa kwa kutupia mipira wavuni, bado Simba haijampata mtu sahihi katika safu ya ushambuliaji.
Jean Baleke si mshambuliaji mbaya lakini hakuweza kuibeba Simba katika michuano mikubwa ikiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika badala yake Baleke ameigharimu Simba katika michuano hiyo kwa namna ambavyo alikuwa akikosa mabao ya wazi.
Baleke ametamba katika Ligi Kuu NBC na michuano mingine lakini pale Simba ilipomtegemea kwenye michuano ya Afrika alishindwa kudhihirisha thamani yake na ndio maana sijashangaa Simba kuachana naye.
Simba hii inamhitaji John Bocco, si huyu wa sasa bali yule wa miaka saba, nane iliyopita, Simba hii inamhitaji Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ yule mwenye rekodi ya mabao katika ligi kuu nchini.
Simba hii inamhitaji Fiston Kayala Mayele, huyu huyu ambaye majuzi alikuwa Yanga na kwa sasa anacheza soka nchini Misri, aina hii ya wachezaji ndio ambao Simba imewakosa.
Msimu huu badala ya kufikiria kuwaacha kina Chama na Ntibazonkiza, wapambane ili wawape wachezaji hao mshambuliaji wa aina ya Mayele huyu wa sasa au Boccco wa miaka ile halafu waone kazi watakayoifanya.
Hii tabia ya kuacha wachezaji kama ilivyokuwa kwa Jonas Mkude kwa kweli inashangaza, Mkude kaenda Yanga kaonesha uwezo wa ajabu, kaibeba pale ilipokuwa na wakati mgumu, mchango huu wa Mkude pengine ungekuwa na maana kubwa Simba.
Naye si mchezaji wa kucheza mara kwa mara lakini unapojua kumtumia Mkude katu hawezi kukuangusha na ndicho ambacho kimedhihirika akiwa na jezi ya Yanga.
Tatizo jingine la Simba ni mafanikio ya Yanga, Simba wanateswa na kushughulishwa mno na mafanikio ya Yanga kuliko matatizo mepesi yaliyo mbele yao.
Simba imecheza robo fainali mara nyingi lakini Yanga kucheza mara moja tu imekuwa tatizo kwa Simba, Yanga imebeba taji la ligi mara tatu na msimu huu mara ya nne, Simba haina amani kama haijawahi kuwa na rekodi ya aina hiyo au haijawahi kubeba taji japo mara mbili mfululizo.
Wakati Yanga na Simba zikiwa hatua ya robo fainali, Simba walishughulika na Yanga kwenye mechi yao na Mamelodi kuliko kujali ugumu wa mechi yao na Al Ahly ya Misri.
Simba wamefungwa na Yanga mabao 5-1, furaha ya Yanga imewatesa na kuwashughulisha na kuna ambao wanateseka hadi sasa kama vile wao hawana rekodi kama hiyo au kubwa kuliko hiyo wakati ukweli ni kwamba wana rekodi kubwa ya mabao sita.
Yanga kucheza fainali Kombe la Shirikisho kumewatesa mno Simba kama vile wao hawajawahi kufikia hatua ya fainali kwenye michuano kama hiyo ya klabu barani Afrika na sijui Yanga wangebeba kombe ingekuwaje?
Ni kweli kwamba klabu hizi zina utamaduni wa kuoneana wivu na kucharurana kwa mafanikio lakini hili la Simba hasa msimu huu limevuka mipaka kiasi cha kusahau mafanikio yao yakiwamo ya hivi karibuni tena kwenye Ligi ya Mabingwa.
Tatizo la tatu ndani ya Simba ni la kiuongozi, mashabiki na hata wanachama kwa sasa hawajui lawama za kinachoonekana kuvurunda kwa timu wamtupie nani kati ya mwenyekiti wa klabu au mwenyekiti wa bodi.
Awali mwenyekiti wa klabu Murtaza Mangungu alionekana kuwa mhanga lakini kuna ambao wamekuwa wakijiuliza hivi karibuni kwamba je aliyekosea ndani ya Simba au anayepaswa kubeba lawama ni Mangungu peke yake?
Tunajua kwamba kuna mashabiki wanaodhani kwamba Simba inahitaji kufumuliwa na kusukwa upya kama vile hilo ni jambo rahisi, katika hili viongozi wawe makini, Simba hii inahitaji mambo machache mno, suala la kuifumua upya linaweza kuwaweka pagumu zaidi ya hapa wanapodhani wako pagumu.
