Barcelona, Hispania
Mpango wa Barcelona ‘Barca’ kumbakisha kocha Xavi baada ya msimu huu unaonekana kugonga mwamba kutokana na kauli ya kocha huyo aliyoitoa kabla ya mechi dhidi ya Almeria kuwachukiza vigogo wa klabu hiyo.
Januari mwaka huu Xavi, 44 alitangaza ataachana na Barca baada ya msimu huu lakini baadaye rais wa klabu hiyo, Joan Laporta alimshawishi aendelee na kibarua hicho na kukawa na kila dalili hizo lakini kauli yake huenda ikaufuta mpango huo.
Akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari, Xavi alizungumzia ugumu wa Barca kupambana kwenye soka la hadhi ya juu akihusisha jambo hilo na masuala ya fedha na sasa Rafael Marquez, kocha wa timu B anatajwa kuchukua nafasi yake.
Xavi ambaye alianza kuinoa Barca Novemba 2021 na kufanikiwa kuipa taji la La Liga msimu wa 2022-23, alisema itakuwa vigumu kwao kupambana kwenye nguvu ya kifedha na mahasimu wao Real Madrid pamoja na timu nyingine kubwa za Ulaya.
“Nafikiri mashabiki wa Barca wanahitaji kuelewa kwamba mazingira ni magumu kweli hasa katika masuala ya kiuchumi ili kuwa na uwezo wa kushindana na Real Madrid nchini Hispania pamoja na timu nyingine za Ulaya,” alisema Xavi.
Xavi hata hivyo alisema kwamba kauli yake hiyo haimaanishi kwamba wataacha kupambana na kupigania mataji bali watajitahidi kuendana na hali hiyo hivyo hivyo lakini hiyo ndiyo hali halisi ya klabu na kwa sasa wanahitaji kuwa imara na kupata muda.

Mahasimu wa Barca, Real Madrid kwa sasa wameshabeba taji la La Liga msimu huu na wapo hatua ya fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya wakisubiri kuumana na Borussia Dortmund hapo Juni Mosi kwenye dimba la Wembley.
Real Madrid pia inadaiwa kuwa katika hatua za mwisho kumsajili mshambuliaji Kylian Mbappe kutoka PSG na wameiacha Barca nyuma kwa tofauti ya pointi 14 kwenye La Liga zikiwa zimesalia mechi mbili kabla ya msimu wa ligi hiyo kufikia tamati.
