Madrid, Hispania
Kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois aliyekuwa majeruhi anatarajia kucheza mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund itakayopigwa Juni Mosi mwaka huu kwenye dimba la Wembley.
Kwa kipindi kirefu cha msimu huu unaoelekea ukingoni, Courtois amekuwa nje ya uwanja baada ya kupata maumivu ya goti mara mbili.
Courtois alirudi uwanjani Mei 4 katika mechi ya La Liga dhidi ya Cadiz lakini baadaye alikosekana katika mechi ya pili ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich.
Tangu wakati huo amekuwa kivutio kwa mashabiki hasa katika mechi dhidi ya Granada na Alaves na katika mechi yake ya mwisho kwenye dimba la Bernabeu, mashabiki walimpa heshima ya kipekee.
Habari za ndani zinadai kuwa benchi la ufundi linaamini kuwa kipa huyo yuko fiti na hakuna ubishi kwamba ataanza mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa hapo Juni Mosi.
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti anaamini Courtois ndiye kipa bora duniani licha ya ukweli kwamba hapendi kulizungumza jambo hilo hadharani.
Kwa upande mwingine kipa huyo amewekwa kando kwenye timu yake ya taifa ya Ubelgiji kwa hoja kwamba hayuko fiti hali ambayo imeacha maswali hasa kwa kuwa Real Madrid inapanga kumtumia kwenye mechi muhimu ya fainali.
Kimataifa Courtois golini fainali Ligi Mabingwa
Courtois golini fainali Ligi Mabingwa
Read also
