Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema pamoja na furaha na anavyojivunia ubingwa wa Ligi Kuu NBC waliotwaa Jumatatu lakini anautoa ubingwa huo kwa mashabiki wote wa timu hiyo.
Gamondi, raia wa Argentina alisema kwamba amefanya hivyo kutokana na sapoti na upendo mkubwa waliowaonesha katika mechi zote walizoshiriki msimu huu.
Yanga iliandika historia ya kubeba ubingwa huo kwa mara ya 30 baada ya kuibutua Mtibwa Sugar mabao 3-1, Uwanja wa Manungu, Morogoro, mechi iliyopigwa Jumatatu iliyopita.
Gamondi alisema walistahili kutwaa ubingwa huo japo ulikuwa mgumu kutokana na ushindani uliokuwepo lakini walionesha wao ni nani na walionesha soka safi na la kuvutia kwa mashabiki zao wote na wapenda soka nchini.
“Najiskia furaha, najivunia lakini ni ubingwa wa Yanga, ni mara yangu ya kwanza kufanya hivi nikiwa na Yanga najivunia sana, tumeonesha sisi ni bora zaidi Tanzania.
“Ubora wetu si kwa ajili ya matokeo tu lakini tumecheza vizuri karibia msimu wote huu, wachezaji wamefanya kazi nzuri, na wale wote waliotusapoti tumefurahi na ningepeda kuupeleka ubingwa huu kwa Wananchi wote Tanzania,” alisema Gamondi.
“Nikiri msimu ulikuwa mgumu, ulianza kwa ugumu maana awali nilieleza wazi tunahitaji ubingwa na tunahitaji kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa, na tulijua haya yote ni magumu na tulihitaji kujiandaa vizuri zaidi ya wapinzani wengine.
“Tulijiamini na wachezaji wengi wazuri waliongezeka msimu huu. Ninachoamini ni kuwa tulitengeneza mashine nzuri ya ushindi, tulishambulia vizuri na tulizuia kwa ustadi mkubwa sana,” alisema Gamondi.
Yanga imetwaa ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo ikiwa na makocha wawili tofauti, awali ilifanya hivyo ikiwa chini ya kocha Munisia, Nassredine Nabi.
Hadi kutwaa ubingwa huo, Yanga imefanikiwa kufikisha pointi 71 dhidi ya Azam FC inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 60 ikifuatiwa na Simba iliyo nafasi ya tatu yenye poiti 57.
