Na mwandishi wetu
Baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Azam jana Alhamisi, kaimu kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema ushindi huo umeongeza morali ya kufanya vizuri kwa timu hiyo kuelekea mechi za lala salama msimu huu.
Mgunda amekiri kuwa walifahamu mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ungekuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao wenye wachezaji wazuri.
Kocha huyo hata hivyo alisema kwamba walifanikiwa kujipanga vyema mazoezini na kufahamu udhaifu wao na hilo liliwasaidia kuibuka na pointi tatu.
“Ushindi huu ni mzuri, utakuwa umeongeza kwa kiasi kikubwa morali ya wachezaji wangu, sababu najua klabu kama klabu ina malengo yake na kikubwa ni kuendelea kupata matokeo, kwa hiyo mpaka mwisho wa ligi tutajua tumefika wapi lakini lengo letu ni kupata matokeo mazuri katika mechi hizi zilizobakia.
“Lakini kikubwa nashukuru Mungu tumepata alama tatu na pili niwashukuru wachezaji wangu kwa kazi kubwa waliyoifanya, sababu tulipeana majukumu maana ilikuwa mechi ngumu, mechi yenye maamuzi ya kuona tunakwenda wapi.
“Ni mechi iliyokuwa na presha na uzito na tulijifua mno kwa kufahamu ubora na udhaifu wao uko wapi lakini tunashukuru tumeshinda, tunajipanga na mchezo ujao,” alisema Mgunda.
Kocha msaidizi wa Azam, Youssouf Dabo alisema: “Kipindi cha kwanza tulitawala vizuri mchezo na wapinzani walikuwa na hali ngumu dhidi yetu, muda mwingine tulikuwa na mipira mingi lakini tulikuwa tunashindwa kufikia lango la wapinzani.
“Kipindi cha pili wapinzani walipoonekana wanataka kufunga tulihitaji kuwa wakakamavu kichwani lakini bahati mbaya baadhi ya wachezaji wanahitaji presha ya mechi nyepesi na hilo haliwezekani maana mechi yenyewe haikuwa rahisi.
Pamoja na ushindi huo kuifanya Simba kufikisha pointi 56 baada ya mechi 25 ikiwa ni pointi moja nyuma ya Azam inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 57 baada ya mechi 26, Simba pia imevunja ubabe wa Azam wa kutofungwa kwenye Ligi Kuu NBC tangu ilipofungwa mara ya mwisho na Namungo mabao 3-1 Oktoba 27, mwaka jana.
