Na mwandishi wetu
Kocha wa Simba aliyeachana na timu hiyo, Abdelhakh Benchikha amesema uamuzi alioutaja kuwa ni mgumu wa kuachana na klabu hiyo hautokani na tatizo lolote la uongozi bali ni tatizo la afya ya mkewe.
Akizungumza kwa lugha ya kiarabu katika taarifa iliyopatikana kwenye mitandao ya klabu hiyo, Benchikha alisema anataka wapenzi na mashabiki wa Simba waelewe kuhusu uamuzi huo aliodai kuwa ni mgumu na ambao hata yeye unamuumiza.
Alifafanua kwamba kuondoka kwake hakutokani na tatizo lolote katika klabu ya Simba badala yake anataka mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo wajue kuwa kocha wao ana tatizo la kifamilia.
“Nataka mashabiki wajue kuwa nina tatizo na tatizo lenyewe nimeliweka wazi ili watu waweze kunielewa vizuri zaidi, ni tatizo la kiafya la mke wangu,” alisema Benchikha.
Benchikha alisema hata viongozi Simba walimuomba asiondoke lakini akaona jambo hilo limekuwa gumu na ndio maana akafikia hatua ya kuchukua maamuzi magumu ambayo yanamuumiza hata yeye.
Alisema kwamba malengo yake na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni kufikia hatua ya nusu fainali au fainali na hata kuchukua kombe lakini hilo halikuwezekana kwa alichokiita kuwa ni mapenzi ya Mungu.
Benchikha hata hivyo alisema timu ya Al Ahly ya Misri waliyopambana nayo katika robo fainali ya ligi hiyo ni timu kubwa japo matumaini yake makubwa yalikuwa ni kuvuka hatua hiyo lakini haikuwa bahati yao,
Hatua ya Benchikha kuachana na Simba imekuja baada ya kuwapo uvumi wa muda mrefu kwamba kocha huyo angeachana na klabu hiyo na hata alipoomba ruhusa na kuondoka kwa muda mfupi kwa kilichoelezwa kuwa ni matatizo ya kifamilia uvumi ulizidi kuenea kwamba asingerudi tena.

Benchikha hata hivyo alirudi nchini na kuendelea na kazi yake na sasa ameiacha Simba ikiwa nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu NBC lakini pia ameiwezesha kubeba taji la Ligi ya Muungano.
Kocha huyo ameondoka na wasaidizi wake wawili, Kamal Boujnane na Farid Zamit na tayari uongozi wa Simba umemtangaza, Juma Mgunda kukaimu nafasi hiyo akisaidiwa na Suleiman Matola.
Mtihani wa kwanza wa Mgunda na Matola utakuwa ni kesho Jumanne katika mechi ya Ligi Kuu NBC dhidi ya Namungo FC itakayopigwa Ruangwa mjini Lindi kwenye Uwanja wa Majaliwa.
