Na mwandishi wetu
Simba imetwaa taji la Ligi ya Muungano baada ya kuichapa Azam FC bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Jumamosi hii usiku kwenye dimba la New Amaan mjini Unguja.
Bao pekee lililoipa Simba taji hilo lilifungwa kwa kichwa na Babacar Sarr katika dakika ya 77 baada ya kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Israel Mwenda, adhabu hiyo ilitolewa baada ya Willy Onana kuchezewa rafu.
Azam licha ya kupoteza mchezo huo lakini walionesha uhai kwa kipindi kirefu na kabla ya bao la Sarr matumaini yaliyokuwapo ni kwa mechi hiyo kufikisha dakika 90 bila bao lolote.
Kwa ushindi huo Simba ambao hilo linakuwa taji lao la kwanza msimu huu, pia wamekabidhiwa kitita cha Sh 50 milioni wakati Azam iliyoshika nafasi ya pili imepewa Sh 30 milioni.
Michuano hiyo iliyoanzia hatua ya nusu fainali pia ilishirikisha timu za KVZ iliyocheza na Simba na Simba kushinda kwa mabao 2-0 wakati Azam katika nusu fainali iliichapa KMKM mabao 5-2.
Ligi ya Muungano inayoshirikisha timu za Tanzania Bara na Zanzibar ilifanyika mara ya mwisho takriban miaka 20 iliyopita na walikuwa ni Simba waliobeba taji mara ya mwisho na sasa ligi hiyo imerudi baada ya maombi ya muda mrefu ya wadau wengi wa soka kutaka ligi hiyo irudishwe.
Soka Simba yabeba taji la Muungano
Simba yabeba taji la Muungano
Read also
