London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema kwamba amekuwa akitafuta ushauri kwa kocha wa zamani wa timu hiyo Arsene Wenger kuhusu kushinda taji la Ligi Kuu England (EPL) kabla ya mechi ya Jumapili dhidi ya Tottenham Hotspur.
Wenger anakumbukwa kwa kuifanyia makubwa Arsenal ikiwamo kubeba mataji ya EPL mara tatu ikiwamo msimu wa 2003-04 ambao mafanikio yake yalikuwa ya kipekee bila kupoteza mechi.
Mwaka 2006 Wenger pia aliweka rekodi kubwa na ya mwisho kwa timu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuifikikisha hatua ya fainali lakini ilikwama mbele ya Barcelona waliobeba taji hilo.
Leo Jumapili, Arsenal itaumana na Spurs katika London Derby, mechi ambayo imebeba hatma ya timu hiyo kwenye mbio za taji la EPL wakati Spurs itakayokuwa nyumbani ikiwa na malengo ya kusaka nafasi katika top four.
Arsenal ndiyo inayoshika usukani wa EPL kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Man City ambayo leo itaumana na Nottingham Forest lakini pia Man City umezidiwa mechi moja na Arsenal.
Arteta ambaye kwa miaka mitano amewahi kuwa mchezaji wa Arsenal wakati Wenger akiwa kocha alisema kwamba mara kadhaa amekuwa akikutana na kujadiliana na kocha huyo kuhusu mambo mbalimbali.
“Nimewahi kuzungumza naye mara chache, kuna baadhi ya mambo kuhusu jinsi walivyobeba taji katika hatua za mwisho mwisho,” alisema Arteta.
