London, England
Man City imeiweka pagumu Arsenal katika mbio za kuliwania taji la Ligi Kuu England (EPL) baada ya kuichapa Brighton mabao 4-0 na kuchupa hadi nafasi ya pili ikiachwa na Arsenal kwa tofauti ya pointi moja.
Arsenal inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 77 katika michezo 34 wakati Man City inayoshika nafasi ya pili hadi sasa imecheza michezo 33 na imebakiza mechi tano kabla ya kuhitimisha mbio za EPL.
Kwa msimamo huo maana yake ni kwamba Mikel Arteta na Arsenal yake ili waweze kulibeba taji la EPL msimu huu si tu kwamba wanatakiwa washinde mechi zao zote zilizobaki bali pia waiombee Man City ipate matokeo mabaya.
Liverpool inayoshika nafasi ya tatu japo si sahihi kuitoa moja kwa moja katika mbio hizo lakini baada ya kupoteza mechi yake na Everton ni kama vile nayo imejiweka pagumu kwani ina pointi 74 katika mechi 34.
Kwa Liverpool nayo si tu kwamba inatakiwa ishinde mechi zake zote zilizobaki bali nayo pia inatakiwa kuiombea Arsenal iteleze na pia inatakiwa ifanye maombi kama hayo dhidi ya Man City.

Kwa jinsi hali ilivyo sasa, vita kubwa zaidi ni kwa Arsenal na Man City na kwa kuwa Man City ina faida ya mechi moja basi haitokuwa ajabu timu hiyo ikifanikiwa kulitetea vyema taji la ligi hiyo.
Man City ikiwa chini ya kocha Pep Guardiola katika mechi yake na Brighton iliyopigwa jana Alhamisi kwenye Uwanja wa Amex, mabao yaliyoipa timu hiyo pointi tatu yalifungwa na Kevin de Bruyne kwa kichwa katika dakika ya 17.
Man City waliongeza mabao mengine mawili yaliyofungwa na Phil Foden katika dakika za 26 na 34 kabla ya Alvarez kufunga ukurasa wa mabao kwa kupachika bao la nne katika dakika ya 62.
